1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden: Afrika inastahili dhima kubwa zaidi duniani

16 Desemba 2022

Rais Joe Biden ameunga mkono hatua ya Afrika kuwa na dhima kubwa duniani na kuapa kuwa mstari wa mbele katika kupigania demokrasia katika bara la Afrika ambalo China na Urusi zinaendelea kupata umaarufu mkubwa.

https://p.dw.com/p/4L2u9
USA Washington | USA-Afrika-Gipfel | US-Präsident Joe Biden
Picha: Kevin Lamarque/REUTERS

Akizungumza katika siku ya mwisho ya mkutano wa kilele wa Marekani na karibu mataifa 50 ya Afrika, Rais Joe Biden amewaambia viongozi hao kwamba Marekani iko pamoja na Afrika kwa lolote lile.

Biden ambaye mnamo mwezi Septemba alitoa wito wa Africakupata kiti cha kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa amesema anaunga mkono pia Afrika ipate nafasi ya kudumu katika kundi la nchi 20 zilizostawi na zinazoinukia kiviwanda - G20.

"Afrika inastahili kuwa katika meza ya kila chumba, kila chumba ambamo changamoto zinazoikabili dunia zinajadiliwa na katika kila taasisi ambayo majadiliano yanafanyika," alisema Biden.

USA Washington | USA-Afrika-Gipfel | US-Präsident Joe Biden
Mkutano wa kilele kati ya Marekani na AfrikaPicha: Kevin Lamarque/REUTERS

Marekani inastahili kutumia fursa zilizopo Afrika

Hapo juzi msemaji wa usalama wa kitaifa wa ikulu ya White House John Kirby alizungumzia umuhimu wa uekezaji wa Marekani barani Afrika na kusema Marekani inatazamia kuwa na mazungumzo ya pande mbili kuhusiana na biashara, uekezaji na fursa za kukua kwa uchumi.

Viongozi wa Afrika wamekubaliana na utaratibu huo. Rais wa Kenya William Ruto amesema Marekani inastahili kutafuta fursa za kuwekeza Afrika kutokana na uwezo mkubwa ilio nao kwa faida ya pande zote mbili.

"Kuna fursa za wazi ambazo Afrika na Marekani zinaweza kuzitumia, tunahitaji kutafuta mbinu ambayo itatuiwezesha sote kunufaika ukizingatia uwezo mkubwa wa ushindani wa Marekani katika mtaji, ujuzi na miundo mbinu na kutumia uwezo wa Afrika wa maliasili, nishati, nguvu kazi na eneo la biashara huria katika bara la Afrika ambalo linatoa fursa ya biashara kufanyika," alisema Ruto.

Rais Ruto amesema inakadiriwa kwamba biashara kilimo barani Afrika itakuwa zaidi ya mara tatu na kufikia dola trilioni 1 ifikapo mwaka 2030 na kwamba mtaji wa Marekani unaweza kutatua tatizo la miundo mbinu Afrika kwa ajili ya ustawi wa bara hilo.

Kenia Nairobi | Feier am Mashujaa Day
Rais wa Kenya William RutoPicha: Simon Maina/AFP

Biashara kati ya China na Afrika ni kubwa mno

Kulingana na uchambuzi wa Kundi la Eurasia, mwaka 2021 biashara kati ya China na Afrika ilikuwa bilioni 254 ikilinganishwa na biashara kati ya Marekani na Afrika iliyokuwa ni dola milioni 64.3 pekee.

Viongozi wa nchi za Magharibi wamekosoa pakubwa kile wanachokiona kama hatua ya China kujikokota katika kulishughulikia suala la mzigo mkubwa wa madeni linalozikabili nchi nyingi za Afrika.

Chanzo: AFPE/Reuters