Biden afanya mazungumzo na viongozi wa Uingereza
10 Julai 2023Biden amefanya mazungumzo ya karibu saa nzima na waziri wa Uingereza Rishi Sunak, huu ukiwa mkutano wa sita baina ya viongozi hao wawili. Kwenye agenda ya mkutano wao vita vya Ukraine vimepewa umuhimu mkubwa, lakini pia wamegusia masuala mengine ya kidunia. Akizungumza katika ofisi ya waziri mkuu wa Uingereza mjini London, Biden amesema uhusiano baina ya Marekani na Uingereza kamwe hautetereki.
''Tumekuwa tukikutana kila mwezi, tulikutana Sam Diego, Belfast, Hiroshima, Washington na hapa. Hakuna rafiki wa karibu wa Marekani zaidi ya Uingereza. Tunayo mengi ya kujadili na nadhani tunaendelea vyema, na tuko katika mwelekeo sahihi. Uhusiani wetu ni imara kama mwamba.''
Tofauti zilijitokeza kati ya Uingereza na Marekani wakati wa tawala za mawaziri wakuu waliomtangulia Rishi Sunak, hasa kutokana na muundo wa biashara kati ya Jamhuri ya Ireland na Ireland ya kaskazini ambayo ni sehemu ya Uingereza.
Soma pia: Biden kukutana na Waziri Mkuu Sunak Jumapili
Baada ya mazungumzo na waziri mkuu Sunak, Rais Joe Biden amesafiri kwa helikopta kutoka katikati mwa mji wa London hadi makao makuu ya mfalme Charles III. Rais huyo wa Marekani hakuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa mfalme huyo, akiendeleza utamaduni wa marais wa Marekani wa kutoshiriki katika sherehe kama hizo. Mazungumzo kati ya mfalme huyo na mgeni wake yalijikita juu ya mipango ya kutunza mazingira.
Biden anatarajiwa kuondoka mjini London jioni ya Jumatatu na kuelekea katika mkutano wa kilele wa NATO unaofanyika katika mji mkuu wa Lithuania, Vilnius. Mada kuu ya mkutano huo utakaodumu kwa siku mbili kuanzia kesho Jumanne, ni juhudi za pamoja za kuisaidia Ukraine kukabiliana na uvamizi wa Urusi, pamoja na uanachama wa Sweden katika jumuiya ya NATO.
Mkutano wa Vilnius unafanyika kukiwapo mitazamo inayokinzana miongoni mwa wanachama wa NATO juu ya uamuzi wa Marekani kuipatia Ukraine silaha tata za mabomu ya mtawanyiko.
Kituo cha mwisho cha ziara hii ya Rais Joe Biden barani Ulaya kitakuwa Finland, nchi ambayo ni mwanachama mpya kabisa wa Jumuiya ya kujihami ya NATO.