Biden aahidi msaada zaidi wa chanjo ya corona kwa Afrika
15 Oktoba 2021Wakikutana katika ikulu ya White House mjini Washington, Biden na Kenyatta waliahidiana kushirikiana kukabili mabadiliko ya tabia nchi na kumaliza machafuko katika pembe ya Afrika.
Biden alitangaza kuwa Marekani itatoa mara moja msaada wa dozi milioni 17 ya Johnson & Johnson kwa Umoja wa Afrika, ikiwa ni nyongeza ya dozi milioni 50 ambazo ilishatoa.
Soma: Bara la Afrika linahitaji haraka chanjo za COVID-19
Biden amesema anatumai chanjo hizo zitasaidia nchi za Umoja wa Afrika. Ameahidi kutoa misaada zaidi ya chanjo dhidi ya COVID-19 kwa Kenya ifikapo mwisho wa mwaka.
Rais Kenyatta ameukaribisha msaada huo akisema zitasaidia kampeni ya utoaji chanjo Afrika.
"Ni furaha kusikia tangazo lako jipya la nyongeza hiyo ya chanjo kwa sababu kama mjuavyo, kama bara tunajikokota nyuma ya mabara mengine kuhusu uwezo wa kuwachanja watu wetu. Kwa hivyo nyongeza yoyote ya msaada kama ambavyo Rais Biden ametaja inakaribishwa sana na tunatumai kushirikiana zaidi,” amesema Rais Kenyatta.
Soma pia: Afrika yaeleza ukosefu wa usawa chanjo za corona katika UNGA
Biden ameahidi lengo jipya, kuzingatia demokrasia, tofauti na mtangulizi wake Donald Trump aliyekuwa karibu na viongozi walioongoza kwa mabavu, lakini pia ambaye hakuficha kutoipenda Afrika.
Kenyatta ndiye kiongozi wa kwanza wa Afrika kuzuru ikulu ya Marekani chini ya utawala wa Biden, mnamo wakati ziara na mikutano ya kilele imepunguzwa kama hatua ya kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona.
Ziara ya Kenyatta ambaye ameahidi kupambana na ufisadi, imejiri mnamo wakati akikabiliwa na ukosoaji kufuatia ufichuzi wa siku chache zilizopita kwenye nyaraka za Pandora uliomtaja yeye na watu sita wa familia yake kumiliki kampuni sita zenye thamani ya dola milioni 30 nje ya Kenya.
Biden hakugusia madai hayo walipozungumza na waandishi wa habari lakini alitoa wito wa kuimarishwa kile alichokitaja kuwa "uwazi katika mifumo ya fedha.” Alimshukuru Kenyatta kwa uongozi wake wa kulinda amani, usalama na demokrasia ya nchi yake na kanda nzima.
"Nchi zetu zinashirikiana kwa dhati kuhakikisha kuna haki, heshima na usawa, na nimejitolea kuimarisha ushirikiano zaidi na Kenya nan chi za Afrika nzima- lakini Kenya ni mshirika muhimu kwa hili," amesema Biden.
Kenya ndiyo inashikilia kwa sasa urais wa kupokezana wa Baraza La Usalama la Umoja wa Mataifa, na imetumia nafasi hiyo kutaka machafuko ambayo yamewaacha maelfu ya watu bila makao na wengi kung'atwa na njaa katika nchi jirani Ethiopia yakomeshwe.
Kenya pia ni mshirika wa muda mrefu wa Marekani katika masuala ya usalama, wakishirikiana karibu kupambana na wanamgambo wa Alshabaab katika taifa jirani la Somalia.
Rais Kenyatta alisema alikuwa anazungumza na Biden kuhusu "vita dhidi ya ugaidi” lakini pia kuhusu mabadiliko ya tabia nchi, kuelekea mkutano wa Umoja wa Mataifa utakaofanyika Glasgow mwezi ujao.
Hata hivyo matumaini ya Kenya ya makubaliano ya kibiashara huenda hayakutimia.
Afisa mmoja wa ngazi ya juu wa Marekani ambaye hakutaka jina lake litambulishwe amesema utawala wa Biden utafanya kazi kwa karibu na Kenya kuhusu biashara lakini akaongeza kwamba bado wanafikiria jinsi ya kushughulikia biashara ya kigeni.
(AFPE, APE)