1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biashara ya watoto

Ursula Berner / Maja Dreyer19 Aprili 2006

Kila siku mia kadhaa ya watoto duniani kote wanaondoka makwao wakiota ndoto ya kuwa na maisha bora, lakini pale panapofika huko waendako wanalazimishwa kuiba au kufanya ukahaba. Wengi wa watoto hawa wanafika Ulaya.

https://p.dw.com/p/CHnT
Watoto wanaofanya kazi katika nchi kigeni
Watoto wanaofanya kazi katika nchi kigeniPicha: TdH

Umoja wa Ulaya sasa umechapisha kitabu kipya kinachohusu uchunguzi mpya juu ya biashara ya watoto, na jinsi ya kupambana na uhalifu huo.

“Biashara ya binadamu kwa jumla ni biashara kubwa sana, hasa biashara ya watoto. Na hiyo ndiyo sababu wanabiashara hawa wa magendo wanakubali kukabiliana na kila hatari na shida kupanga safari hizo na kuzipata karatasi zote zinazohitajika, kwani katika biashara ya watoto mapato ni makubwa kama vile katika biashara ya madawa ya kulevya ambayo ni moja ya biashara kubwa zaidi duniani.”

Anayesema haya ni Claire Potaux, mtaalamu wa mambo ya biashara ya binadamu katika shirika la kimataifa la uhamiaji. Akiwa ni mmoja wa wahariri wa kitabu kipya kuhusu biashara ya watoto barani Ulaya analenga kuongeza maarifa juu ya biashara huyo. Kwa mujibu wa Bibi Potaux, watu wengi katika nchi za Ulaya wana picha fulani wakiwafikiria wahanga wa biashara ya watoto, yaani msichana wa miaka 16 hivi aliyelazimishwa kufanya kazi kama malaya. Lakini kuna njia nyingi ya kuwanyonya watoto hawa. Kusini wa Ulaya huwa wanafanya kazi katika nyumba za watu wengine bila ya kuwa na haki zozote au wanatumwa barabarani kuombaomba. Watoto wengi wanatumiwa kuuza sehemu ya ndani ya miili yao kama mafigo. Vitendo vinavyoripotiwa zaidi na vyombo vya habari ni picha za uchi za watoto wa kila umri au ukahaba wa watoto hawa katika mabaa au barabarani.

Claire Potaux amesema: “Biashara ya watoto siyo tu uhalifu uliopangwa bali pia ni ni uhalifu dhidi ya haki za kimsingi za binadamu. Kwa watoto ni tukio baya mno wakipelekwa katika nchi za kigeni bila ya mawasiliano yoyote na jamaa zao na bila ya kuweza kwenda shule tena. Juu ya hayo, wanabiashara wa binadamu ni watu wakali sana. Watoto hupigwa, hutishwa na hushurutishwa kutafuta fedha, ikiwa ni kwa kuiba, kuombaomba au kuuza miili yao. Hata ikiwa idadi ya vitendo kama hivi vinavyojulikana si kubwa, hata hivyo ni muhimu kuupiga vita uhalifu huo mbaya.”

Claire Potaux na wataalamu wengine wanasisitiza pia kwamba ni muhimu wahanga wa biashara ya watoto watendewe vizuri na polisi. Kuwarudisha tu makwao si suluhisho linalofaa, kwani baada ya muda fupi watauzwa tena katika nchi nyingine. Kwa sababu hiyo, shirika la kimataifa la uhamiaji lilianzisha mradi wa kuwarudisha watoto makwao na kuwasindikiza huko ili waweze kwenda shula na kuanza maisha mazuri kwa watoto wanaokubali mradi huo. Wengine ambao hawawezi kurudi makwao watasaidiwa hapa barani Ulaya.

Tatizo kubwa zaidi la biashara ya watoto ni umaskini katika nchi nyingi za dunia unaowasababisha wazazi kuwatuma watoto wao katika nchi tajiri ili wapate fursa nzuri na waweze kuzisaidia familia zao. Bila ya tatizo hilo kuondoshwa biashara ya watoto itaendelea.