1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biashara huria na democrasia magazetini

Oumilkheir Hamidou
19 Januari 2017

Mvutano kati ya China na Marekani kuhusu biashara ya kimataifa, hotuba ya kuaga ya rais Joachim Gauck na laana kwa yaliyosemwa na Björn Höcke wa chama cha AfD kuhusu Holocaust ndio mada zilizogonga vichwa vya habari

https://p.dw.com/p/2W2QY
Deutschland Abschiedsrede von Bundespräsident Gauck
Picha: Reuters/H. Hanschke

Tunaanzia  katika milima ya Davos nchini Uswisi linakofanyika kongamano la kimataifa la kiuchumi ambako rais wa China Xi Jinping alikumbusha umuhimu wa kuendelezwa biashara ya kimataifa, hotuba iliyoangaliwa kama onyo kwa rais mteule wa Marekani Donald Trump. Gazeti la masuala ya kibiashara Handelsblatt la mjini Düsseldorf, linachambua misimamo ya China na Marekani kuelekea biashara ya kimataifa na kuandika: "Anaeamini kwamba China inaweza kuiacha kando Marekani na kugeuka kuwa mlinzi wa mwongozo wa uchumi huria duniani, ameshindwa kuutambua ukweli wa hali ya mambo katika biashara jumla duniani. Bila ya shaka China inapigania biashara huru , lakini kwa wakati wote ambao wao ndio wanaofaidika. Kinyume na Marekani katika enzi za kabla ya Trump, Beijing haijawahi kudai jukumu la kulinda muongozo jumla wa kiuchumi, unaopindukia masilahi yake. Kila nchi inastahiki kuridhika kwa upande wake. Naiwe waimla, taifa linaloongozwa na chama kimoja au taifa linalofuata mfumo wa demokrasia, yote hayo hayana umuhimu wowote kwa wakati wote ambao kila mmoja anafaidika. Mfumo wa China ambao ni mchanganyiko wa ubepari na uimla unadhihirisha tu kwamba maendeleo ya kiuchumi yanawezekana hata kama nchi haifuati mfumo wa kidemokrasi. Mwisho wa mfumo kama huo lakini hakuna anaeujua.

Demokrasia ilindwe anasema Joachim Gauck

Rais wa shirikisho la jamhuri ya Ujerumani Joachim Gauck ameamua kutogombea mhula wa pili madarakani. Katika hotuba yake ya mwisho katika kasri la Bellvue mjini Berlin, rais Gauck amesema demokrasia inahujumuia. Ametoa wito wa kuitetea. Gazeti la mjini Berlin,"Berliner Zeitung" linaandika: "Ni dhahir kabisa kwamba Joachim Gauck, kutokana na matukio ya miaka ya hivi karibuni, anamaliza mhula wake akiwa na matumaini haba ikilinganishwa na yale aliyokuwa nayo alipokabidhiwa wadhifa huo mwezi Marchi mwaka 2012. Matatizo mengi aliyoyataja mwanzoni mwa mhula wake yamezidi makali badala ya kupungua. Shaka shaka kuelekea umoja wa Ulaya, hatari zinazosababishwa na itikadi kali, watu kupoteza imani kutokana na mageuzi ya kila aina-yote hayo yalikuwa pia miongoni mwa masuala aliyokuwa akiyazungumzia miaka mitano iliyopita. Alitaka kuwapa watu moyo na kuwaondolea hofu, kama alivyofanya jana katika kasri la Bellevue alipokosoa desturi mbaya za woga, kutojali na kutojiamini. Tusitaharuki".

AfD walaaniwa kwa yaliyosemwa na Björn Höcke

Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu matamshi ya mwenyekiti wa kundi la wawakilishi wa chama cha Chaguo Mbadala kwa Ujerumani AfD katika bunge la jimbo la Thuringia, Björn Höcke dhidi ya makumbusho ya wahanga wa mauwaji ya halaiki ya wayahudi Holocaust mjini Berlin yamelaaniwa na kila upande. Gazeti la Frankenpost linaandika: "Si jambo linalovumilika kusikia matamshi yaliyokuwa yakitolewa na watawala wa ujamaa wa kizalendo NS yanasikika nchini Ujerumani. Björn Höcke, tangu fikra zake, mwende wake mpaka vitendo yake si chengine isipokuwa vya kueneza hisia za kibaguzi. Katika baadhi ya maeneo AfD wanaweza kutegemea uungaji mkono wa  asili mia 20 ya wapiga kura. Kilio cha wanasiasa kilihanikiza jumanne iliyopita, korti ya katiba ilipoamua kutokipiga marufuku chama cha NPD. Chama cha AfD kina ushawishi mkubwa zaidi na kinazidi kuwavutia wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia. Hatari inayotokana na makundi yanayopinga demokrasi ni kubwa zaidi kuliko ile ya NPD katika zama zake.

 

Mwandishi: Hamidou Oumilkheir

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman