Besigye amuonya Museveni asijaribu kubadili tena katiba
11 Julai 2017
Kwa sasa, idadi kubwa ya wabunge wamezima simu zao za mkononi au kutokuzipokea pale wanapopigiwa, wakihofia kukosolewa na kushutumiwa pamoja na rai za wananchi za kuwataka wasishiriki katika kubadili katiba ya nchi ili kuondoa Ibara Nambari 102 inayoweka kikomo cha umri wa kugombea ambapo mtu aliyetimu miaka 75 anazuiwa kuwania urais.
Kampeni hii inafanyika kwenye mitandao ya kijamii ambapo nambari zote za simu za wanasiasa zimeorodheshwa.
Kwa sasa Rais Museveni ana umri wa miaka 74, hivyo kulingana na katiba hawezi kugombea wadhifa wa urais ambao ameushikilia tangu mwaka 1986.
Kiongozi wa upinzani, Kizza Besigye, amewaonya wabunge kutokubali mchakato wowote wa kupiga kura kuhusu suala hilo na kuwataka wafahamu kuwa "Rais Museveni na wafuasi wake watafanikisha hila yao."
Hata hivyo, wanasiasa wa chama tawala NRM wanaounga mkono kwa dhati hatua itakayomwezesha Museveni kugombea urais wana mtazamo kuwa katiba ni chombo hai ambacho kimefanyiwa mageuzi mara kadhaa kulingana na hali ya kisiasa, pia wakihoji kuwa "kikomo kwa umri si hoja katika mataifa mengi duniani."
Ifahamike kuwa mwaka 2005, bunge lilipitisha mswaada wa kuondoa kipengele cha rais kuongoza kwa awamu mbili tu kama ilivyo katika mataifa ya Kenya na Tanzania. Hii ilimwezesha Rais Museveni kugombea tena urais.
Besigye amewashauri Waganda kupinga vikali hatua ya kuondoa ibara ya pekee "inayomzuia Museveni kuongoza Uganda baada ya mwaka 2021."
"Hiyo ndiyo njia ya pekee kuepusha kuwa na rais wa maisha na kufungua sura mpya ya kidemokrasia itakayowezesha mchakato wa kupokezana madaraka kwa njia isiyo ya umwagikaji damu kama ilivyokuwa wakati Museveni alipochukua madaraka," anasema mgombea huyo wa mara tatu wa urais.
Besigye anapendekeza utawala wa mpito utakaojumuisha wadau wote wa kisiasa na kijamii katika awamu ya kwanza baada ya rais Museveni kuondoka madarakani.
Kwa upande wao, wanasiasa wa chama tawala wanasisitiza kuwa Museveni angali kipenzi cha raia wa Uganda na kwa hiyo apewe fursa ya kutekeleza mipango yake kabambe ya kiuchumi kama vile uzalishaji wa mafuta.
Wiki iliyopita, Waziri wa Katiba Jenerali Kahinda Otafire aliwasilisha mswaada husika na bunge linatarajiwa kuanza kuushughulikia mara moja.
Mwandishi: Lubega Emmanuel/DW Kampala
Mhariri: Mohammed Khelef