Besigye akamatwa tena
22 Februari 2016Besigye, ambaye amekataa kuyatambua matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika siku ya Alhamis (Februari 18) na ambayo yalimpa ushindi Rais Yoweri Museveni, alichukuliwa na polisi siku ya Jumatatu (Februari 22), siku ambayo alikuwa ametoa wito kwa wafuasi wake kuandamana nchi nzima.
Polisi inasema maandamano hayo ni haramu, wakiongeza kwamba kwa kuwa muhula mpya wa masomo unaanza, "basi maandamano hayo yangeliingilia haki za wazazi na watoto wao wanaokwenda skuli."
Besigye aliwekwa kwenye kizuizi cha nyumbani siku ya Ijumaa baada ya polisi kuyavamia makao makuu ya chama chake, Forum for Democratic Change (FDC), wakiwatuhumu maafisa wa chama hicho "kutaka kutoa matokeo yao ya kura kinyume cha sheria."
Polisi walimchukuwa Besigye kutoka nyumbani kwake Kasangati, kaskazini mwa mji mkuu Kampala na kumpeleka kwenye kituo cha polisi cha Nagalama, kwa mujibu wa msemaji wa polisi, Patrick Onyango.
Besigye hakusema kitu wakati akitupwa kwenye gari lenye vioo vya giza na kuondolewa nyumbani kwake na Onyango hakutoa ufafanuzi zaidi.
'Nyumba imekuwa kambi ya kijeshi'
Mke wa Besigye, Winnie Byanyima, ambaye pia ni mkurugenzi mtendaji wa shirika la misaada la Oxfam International, alituma picha kwenye mtandao wa Twitter ikiwaonesha polisi wa kuzuia fujo nje ya nyumba yao, akisema: "Nyumba imekuwa kama kambi ya kijeshi. Tunataka amani."
Matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi siku ya Jumamosi yalimpa Museveni asilimia 70 ya kura dhidi ya asilimia 30 za Besigye, ambaye hadi matokeo hayo yanatangazwa alishakamatwa mara tatu, kabla, wakati na baada ya uchaguzi.
Hadi sasa, Besigye ameshindwa mara ya nne kwenye uchaguzi wa urais na kila mara amekuwa akilalamikia wizi wa kura na kila mara maandamano ya wafuasi wake yamekuwa yakikabiliwa na ukandamizaji mkubwa wa vyombo vya dola.
Museveni, ambaye ameitawala Uganda tangu mwaka 1986, aliusifia ushindi wake na akayatupilia mbali malalamiko ya Besigye na zile za waangalizi ambao wameuita uchaguzi huo kuwa "haukuwa wa haki wala huru".
"Wapinzani si viongozi. Ni watu domokaya, waongo, wanasemasema tu," alisema kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 71 siku ya Jumapili.
"Na hao Wazungu hawako makini," alisema akikusudia waangalizi wa Umoja wa Ulaya waliosema kuwa Tume ya Uchaguzi ya Uganda haikuwa na uwazi na kwamba polisi walitumia nguvu kupita kiasi dhidi ya upinzani.
Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/dpa
Mhariri: Saumu Yussuf