1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Besigye akamatwa akichunguza uchakachuaji wa kura

18 Februari 2016

Mgombea wa chama kikuu cha upinzani nchini Uganda Kizza Besigye alikamatwa na polisi baada ya uchaguzi uliyokumbwa na ucheleweshwaji na makabiliano kati ya polisi na waandamanaji wenye hasira. Aliachiwa bila mashtaka.

https://p.dw.com/p/1Hxkw
Uganda Rukungiri Kizza Besigye beim Wahllokal
Mgombea wa FDC Kizza Besigye akiwa na wafuasi wake.Picha: Getty Images/AFP/STRINGER

Chama cha Besigye cha Forum for Democratic Change FDC, kilisema mgombea wake alikamatwa baada ya kwenda eneo la Naguru kuchunguza kituo haramu cha kukusanya matokeo katika wilaya yake ya nyumbani kilichokuwa kinasimamiwa na chama tawala cha National Resistance Movememt NRM.

"Aliingia na kuwaona wakiweka alama ya ndiyo kwenye karatasi za kura kabla. Walimkamata na kumpeleka eneo lisilojulikana," alisema afisa mwandamiziwa FDC Shawn Mubiru. Lakini wakili wake Ladislaus Rwakafuzi alisema Besigye aliachiwa baada ya muda mfupi bila kufunguliwa mashtaka yoyote.

Hakukuwa na uthibitisho kutoka kw ajeshi la polisi, lakini Besigye amekuwa akikamatwa mara kwa mara na polisi huko nyuma, na kisha kuachiwa bila mashtaka saa chache baadae. Waangalizi wa uchaguzi wa kimataifa wakati huo walionya kuwa kuchelewesha kuwasilishwa klwa vifaa vya uchaguzi kwa masaa mengi kutasababisha kukosa imani na mchakato huo, ambapo baadhi ya wapigakura waliovunjwa moyo na wafuasi wa upinzani waliwalaumu maafisa kwa kukwamisha mchakato huo kwa maksudi.

Upigaji kura katika uchaguzi wa rais na bunge nchini Uganda ulichelewa kuanza kwa masaa kadhaa katika vituo kadhaa katika maeneo ya mjini na wilaya jirani ya Wakiso, ambako masanduku ya kura na karatasi havikuwasilishwa katika muda muda stahili. Mji mkuu wa Uganda kwa kawaida ni ngome ya upinzani.

Wapigakura wengi mjini Kampala walichelewa kuanza kupiga kura.
Wapigakura wengi mjini Kampala walichelewa kuanza kupiga kura.Picha: picture-alliance/AP Photo/B. Curtis

"Ucheleweshaji wa rasili moja au mawili unaweza kueleweka. Lakini ucheleweshaji wa masaa matatu, manne, matano na hata sita, hasa katika mji mkuu wa Kampala hausameheki kabisaa na hautasaidia kuujengea imani mfumo na mchakato wote," alisema Olusegun Obasanjo, mkuu wa kundi la waagalizi kutoka Jumuiya ya Madola nchini Uganda.

Uchaguzi wa ushindani

Rais Yoweri Museveni anakabiliwa na changamoto kutoka kwa wagombea saba wa upinzani, lakini anatazamiwa na wengi kuushinda uchaguzi huo kwa muhula wa tano, ambapo mpiganaji huo wa zamani wa vita vya msituni ataingia katika muongo wake wa nne madarakani.

Baada ya kupiga kura yake magharibi mwa nchi Museveni mwenye umri wa miaka 71 alisema anakwenda kupumzika. "Nilikuwa silali," alisema. "Kesho nitakwenda kufanya matembezi yangu marefu nifanye mazoezi na kisha niende kuwatazma ngombe wangu." Aliongeza kuwa yeyote atakaevuruga uchaguzi "atawekwa katika jokofu" ili apowe.

Zoezi la kuhesabu kura lilianza wakati wengine wanaendelea kusubiri kupigakura kwenye foreni katika mji mkuu Kampala, ambako zoezi la kupiga kura lilisogezwa hadi usiku. "Watu wana hasira na kila mmoja anaamini kuna njama nyuma ya haya kutokana na namna wanavyochelewesha mchakato mzima," alisema Moses Omony, dereva wa pikipiki. "Tunajua hili linafanywa kwa maksudi," alisema Marius Nkata, fundi ujenzi.

Washindani wakuu wa kinyanganyiro cha urais - Amama Mbabazi, Kizza Besigye na Yoweri Museveni.
Washindani wakuu wa kinyanganyiro cha urais - Amama Mbabazi, Kizza Besigye na Yoweri Museveni.Picha: DW/Reuters/picture-alliance/dpa

Mbabazi asema tume ilikusudia

Tume ya uchaguzi ilisema awali kuwa inasikitika kwa ucheleweshaji huo katika baadhi ya maeneo na kuomba kuwepo na utulivu, lakini mgombea wa upinzani Amama Mbabazi, waziri mkuu wa zamani na mkereketwa wa chama tawala, aliilaani tume hiyo. "Tunahofu kwamba hatua hizo ni za maksudi na hakuna sababu yoyote ya kuhalalisha ucheleweshaji huo," ilisema taarifa ya mkuu wa shughuli za Mbabazi Solome Nakaweesi.

Mitandao ya kijamii kama vile Facebook na Twitter, ilikuwa haipatikani kwa sehemu kubwa siku ya uchaguzi ingawa Waganda waliokubuhu katika matumizi ya intanet walikwepa uzuwiaji huo kwa kutumia mitandao binafsi. Mamlaka ya mawasiliano ya Uganda UCC, ilisema kuzimwa kwa mitandao hiyo kulifanyika kwa sababu za kiusalama, lakini bila kutoa maelezo zaidi.

Zaidi ya Waganda milioni 15 waliandikishwa kupiga kura katika vituo zaidi ya 28,000 kwa nafasi za rais, bunge na madiwani, ambapo viti 290 vya ubunge vinagombaniwa na wawakilishi kutoka vyam 29 vya kisiasa. Zaidi ya askari polisi 150,000, wanajeshi na maafisa wengine wa usalama waliwekwa kuhakikisha usalama kulingana na maafisa wa uchaguzi.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/adpe,afpe

Mhariri: Daniel Gakuba