1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Berlusconi akanusha kauli kuhusu kambi za mateso Ujerumani

Josephat Nyiro Charo29 Aprili 2014

Berlusconi amedai Ujerumani haitambui kuwepo kwa kambi za mateso wakati wa utawala wa manazi. Wachambuzi wanaiona kauli ya Berlusconi aliyoitoa wakati wa kampeni kama jitihada ya mwisho kujinusuru kisiasa.

https://p.dw.com/p/1Bqg1
zur Nachricht - Neuer Berlusconi-Prozess
Picha: picture-alliance/AP

Waziri mkuu wa zamani wa Italia, Silvio Berlusconi amekanusha kwamba yeye ni mtu anayeipinga Ujerumani, baada ya kusababisha fedheha mwishoni mwa juma lililopita kwa kudai kwamba Ujerumani haikutambua kuwepo kwa kambi za mateso wakati wa utawala wa wanazi.

Berlusconi amesema wapinzani wake wa mrengo wa shoto wameitafsiri vibaya kauli yake aliyoitoa kumhusu Martin Schulz, raia wa Ujerumani ambaye ni rais wa bunge la Ulaya na ambaye ni mgombea wa vyama vya mrengo wa shoto katika kuwania wadhifa wa rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya. Kwenye mkutano wa kampeni wa chama chake cha Forza Italia Jumamosi iliyopita, mjini Milan, Berlusconi alimueleza Shulz, ambaye aliwahi kumlinganisha na msimamizi wa kambi ya mateso, kama adui wa Italia.

Lakini Berlusconi amesema alikuwa akijaribu kumsaidia Schulz apate ajira mwaka 2003. Wakati huo aliibua kashfa katika bunge la Ulaya wakati aliposema katika hotuba yake mbele ya wabunge kuwa Shulz angefaa katika jukumu la msimamizi wa kambi ya mateso kwenye filamu. Kwa mujibu wa shirika la habari la Italia, Ansa, safari hii Berlusconi ameuchochea moto tena akisema "Sikutaka nimuudhi Schulz lakini kwa jina la Mungu kwa Wajerumani kambi za mateso hazikuwepo."

Katika taarifa yake Berlusconi amejitetea akisema, "Ni ugomvi kuielekeza kwangu dhana yoyote dhidi ya Ujerumani au ukatili wowote wa kudhania tu dhidi ya Wajerumani, ambao ni marafiki zangu."

Ujerumani yakasirishwa na kauli ya Berlusconi

Serikali ya Ujerumani imepuuzilia mbali kauli ya Berlusconi ikiitaja kuwa ya kipumbavu. Steffen Seibert, Msemaji wa kansela wa Ujerumani Angela Merkel, amewaambia waandishi wa habari mjini Berlin jana kwamba madai ya Berlusconi yalikuwa ya kipuuzi mno kiasi kwamba serikali ya Ujerumani haitatoa kauli yoyote kuyahusu.

Steffen Seibert PK Merkel Unfall 06.01.2014
Steffen Seibert, Msemaji wa kansela wa UjerumaniPicha: picture-alliance/dpa

Ikumbukwe kwamba Ujerumani huandaa kumbukumbu za kila mwaka kwa ajili ya wahanga wa mauaji ya wayahudi, Holocaust, na masomo ya historia huweka mkazo juu ya uhalifu uliofanywa na Wajerumani dhidi ya wayahudi na makundi mengine madogo ya watu wakati wa utawala wa manazi.

Katibu mkuu wa chama cha Social Democratic, SPD, nchini Ujerumani, Yasmin Fahimi, ameyaeleza matamshi ya Berlusconi kama ya kuudhi, ya kipuuzi na yasiyokubalika kabisa. Fahimi aidha amesema matamshi hayo hayakuitia doa sifa ya Italia bali pia yanauhatarisha utamaduni na maadili ya kisiasa ya Ulaya.

Mgombea wa wadhifa wa urais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya wa chama cha European People's Party, EPP, Jean Claude Junker, ambaye ni waziri mkuu wa zamani wa Luxembourg, amemtaka Berlusconi aombe radhi na ayafutilie mbali matamshi yake kuhusu kambi za mateso akisema yamemghadhabisha.

Mwandishi: Josephat Charo/RTRE/DPAE

Mhariri: Yusuf Saumu