Berlusconi ahukumiwa kifungo
7 Machi 2013Kwa mujibu wa sheria za mfumo wa kisheria nchini Italia ina maana kuwa kiongozi huyo wa zamani tajiri mwenye umri wa miaka 76 , hatahitajika kwenda jela hadi pale hatua za rufaa zitakapofikia mwisho, na mahakama ya juu huenda bado ikabadilisha uamuzi huo.
Hatua hii imekuja katikati ya mkwamo mkubwa wa kisiasa unaojitokeza kutokana na kutofikisha mwisho hatua za uchaguzi wiki iliyopita , uchaguzi ambao haukutoa kwa chama chochote uwezo wa kuunda serikali kwa wingi ilionao , licha ya kuwa muungano wa Berlusconi wa nadharia za mrengo wa wastani kulia ulijitokeza kuwa ni nguvu ya pili katika bunge.
Akabiliwa na kesi nyingi
Berlusconi anakabiliwa na mlolongo wa kesi , huku kesi tofauti kuhusiana na madai ya kukiuka kulipa kodi na kumlipa msichana mwenye umri mdogo fedha kwa madhumuni ya kufanya nae ngono ikikaribia kufika mwisho mwezi huu.
Amekana kuwa hana hatia ya kufanya kitu chochote kinyume na sheria katika kesi hiyo na hukumu hii imekosolewa na wakili wake Piero Longo, ambaye mara nyingi amemshutumu jaji Milan kuhusiana na keshi kadha zinazomkabili Berlusconi katika miaka kadha.
"Sikushangazwa kutokana na kwamba ni Milan na inamhusu Berlusconi," amewaambia waandishi habari baada ya hukumu hiyo.
"Lakini nina wasi wasi na kushutushwa kwasababu nina hakika kabisa kuwa madai dhidi ya Berlusconi yalikuwa dhaifu na yenye utata na hata kuwa hayakustahili kuwapo kabisa".
Kaka yake Berlusconi Paolo , mkuu wa gazeti linalomilikiwa na familia hiyo la Giornale Daily , amehukumiwa kwenda jela miaka miwili na miezi mitatu kuhusiana na kesi hiyo hiyo, ambayo imehusika zaidi na maelezo yaliyonaswa kwa siri , yanayohusu ununuzi wa benki , maelezo ambayo yalichapishwa katika gazeti hilo.
Fidia
Mahakama pia imempatia kiasi cha euro 80,000 kama fidia Piero Fassino , ambaye alikuwa mkuu wa chama cha mrengo wa wastani kushoto katika wakati wa tukio hilo na ambaye matamshi yake yalinaswa katika ukanda na kuchapishwa katika gazeti hilo.
Fassino amesisitiza kuwa Giornale, ambalo ni gazeti la mrengo wa kulia lilichapisha maelezo hayo muda mfupi kabla ya uchaguzi wa mwaka 2006 ili kujenga mazingira kuwa Fassino amechukua hatua ambazo zinaweka mbinyo katika ununuzi wa benki ya Banca Nazionale del Lavono kwa kampuni ya bima ya Inipol mwaka 2005.
Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Yusuf, Saumu