BERLIN.Serikali kuongeza bajeti kwa ajili ya kupambana na ufashisti mambo leo
23 Oktoba 2006Polisi mjini Berlin wamewakamata mafashisti mamboleo 16 miongoni mwa 750 waliokusanyika nje ya jela kudai kuachiwa mwanamuziki wa bendi iliyopigwa marufuku ya wafuasi wa kifashisti mambo leo.
Michael Regener anaetumikia kifungo cha zaidi ya miaka mitatu alihukumiwa mwaka 2003 baada ya kupatikana na hatia ya kuimba nyimbo zinazoeneza chuki dhidi ya wayahudi na wageni.
Maandamano hayo yaliandaliwa na chama cha mrengo mkali wa kulia cha NDP kinacho wakilishwa katika mabunge mawili ya mikoa ya Ujerumani Mashariki.
Balozi wa Israel nchini Ujerumani Shimon Stein ameonya dhidi ya hatari ya kupuuza makundi ya mrengo mkali wa kulia.
Serikali ya Ujerumani imesema itaongeza bajeti kwa kiasi cha Euro milioni tano zaidi kukabiliana na hatari ya ufashisti mambo leo.