1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BERLIN:Muda wa wanajeshi wa Ujerumani nchini Lebanon kurefushwa

22 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBWr

Baraza la mawaziri wa serikali kuu ya Ujerumani limeidhinisha hii leo mpango wa kurefushwa muda wa wanajeshi wa Bundeswehr wanaolinda amani nchini Lebanon.

Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Franz Josef Jung amesema kwamba jukumu hilo litadumu hadi Februari mwakani.

Mawaziri hao wameidhinisha kuendelea kuwepo mashua nane za kijeshi katika pwani ya Lebanon ili kuzuia biashara haramu ya silaha zinazoingizwa kinyume cha sheria na wanamgambo wa Hezbollah.

Kwa sasa wapo wanamaji wa Kijerumani 960 wanaopiga doria katika fukwe za pwani ya Lebanon lakini huenda idadi ya askari hao ikapunguzwa.

Bunge la shirikisho la Bundestag linatazamiwa kuupigia kura mswaada huo mwezi ujao.

Wanamaji wa Ujerumani wanaongoza shughuli za kikosi cha umoja wa mataifa cha kulinda amani tangu kumalizika kwa vita baina ya jeshi la Israel na wanamgambo wa Hezbollah vya msimu wa kiangazi wa mwaka jana.