Berlin:Mbunge kufukuzwa chamani kwa kuwakosoa Wayahudi:
11 Novemba 2003Matangazo
Vyama ndugu vya Christian Democratic (CDU) na Christian Social (CSU) nchini Ujerumani leo vimeanza harakati za kutaka kumfukuza chamani Mbunge Martin Hohmann. Uamuzi kamili utachukuliwa na Wabunge wa vyama hivi viwili siku ya Ijumaa. Viongozi wa vyama hivi wakikutana chini ya Mwenyekiti wao Bibi Angela Merkel, wamesema hapo kabla kuwa Mbunge Hohmann, kutokana na hotuba yake aliyoitoa inayowakosoa Wayahudi, anapaswa kufukuzwa kwenye uongozi na chamani. Viongozi wa CDU na CSU wanasema kuwa Mbunge huyo wa chama cha CDU katika mkoa wa Hesse anapaswa kuwajibika kutokana na usemi wake kuwa Wayahudi ni "Umma ulioshiriki katika kufanya Maovu." Utaratibu wa kumfukuza chamani, kwa mujibu wa Kiongozi wa CDU na mkuu wa mkoa wa Hesse, Bw. Roland Koch, utaendeshwa katika mkoa wake. Hohmann, ikiwa atafukuzwa chamani, ataendelea kuwa Mbunge wa kujitegemea.