BERLIN:Bi Merkel asisitiza umuhimu wa kupambana na athari za hali ya anga
1 Machi 2007Kansela wa Ujerumani Bi Angela Merkel anatoa wito wa kuchukua hatua madhubuti za kupambana na atahari za mabadiliko ya hali ya anga.Wito huo unatolewa wakati kiongozi huyo alipohutubia Bunge mjini Berlin hii leo na kushawishi wabunge wa Umoja wa Ulaya kuidhinisha malengo ya kupunguza viwango vya gesi za viwanda.
Bi Merkel anaeleza kuwa Umoja wa Ulaya unapaswa kuwa mfano kwa mataifa mengine ulimwenguni.Nchi ya Ujerumani ni mwenyekiti wa Umoja huo kwa sasa vilevile Kundi la mataifa nane yaliyostawi kiviwanda Ulimwenguni G8.Mawaziri wa Umoja huo walitangaza mpango wa kupunguza viwango vya gesi za viwanda kwa asilimia 20 ifikapo mwaka 2020 ikilinganishwa na viwango vya maika ya tisini.Hatua hiyo sharti iidhinishwe na mataifa wanachama katika mkutano wa wiki ijayo mjini Brussels nchini Ubelgiji. Bi Merkel anaipa kipa umbele suala hilo nyeti la mabadiliko ya hali ya anga katika majukumu yake kama kiongozi wa Umoja wa Ulaya vilevile kundi la G8.
Viongozi wa Ulaya kwa upande wao wanataraji kuwa baada ya muda Marekani na mataifa yanayoendelea kama India yatajihusisha na vita hivyo vya kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya anga.Kansela huyo wa Ujerumani kwa upande mwingine anatia juhudi kufikia makubaliano katika mazungumzo ya biashara ya Doha yatakayowezesha utandawazi.