Berlin yampokea Obama kwa ulinzi mkali
19 Juni 2013Baada ya kuondoka katika mkutano wa viongozi wa kundi la mataifa nane yaliyoendelea kiviwabda G8 mjini Belfast, Ireland ya Kaskazini, Obama alitua kwa ndege yake ya Air Force One katika uwanja wa ndege wa Tagel mjini Berlin majira ya saa mbili jioni, akisindikizwa na mkewe Michell na mabinti zao wawili. Usalama wa mji huo mkuu wa Ujerumani umeimarishwa zaidi wakati wa ziara hii ambapo askari polisi 8,000 wamepelekwa kuhakikisha hakuna jambo lolote baya linalotokea.
Obama atafanya mazungumzo leo na Kansela Angela Merkel, kabla ya kutoa hotuba kwa hadhira ya waalikwa tu katika uwanja wa Pariser uliyoko mbele ya Geti la Brandenburg, ambao ni eneo maalumu katika historia ya urafiki wa Ujerumani na Marekani. Pia atakutana na rais wa Ujerumani Joachim Gauck, na mgombea wa kiti cha ukansela kwa tiketi ya chama kikuu cha upinzani, SPD Peer Steinbrück.
Maafisa mjini Berlin walisema Obama atahutubia hadhira ya wageni waliochaguliwa 4,000, lakini gazeti moja limesema orodha hiyo iliongezwa na kufikia majina 6,000 baada ya kupata idhidi kutoka mjini Washington. Hotuba ya Obama inakuja karibu miaka 50 baada ya hotuba maarufu iliyopewa jina la 'Ich bin ein Berliner" iliyotolewa na mtangulizi wake rais John F. Kennedy.
Sakata la udukuzi wa mawasiliano
Wakati maafisa kutoka pande zote wamesisitiza kuhusu uhusiano wa kihistoria uliopo baina ya Marekani na Ujerumani, ziara ya Obama imekuja wakati ambapo Wajerumani wengi wanapaza sauti za ukosoaji, kuhusiana na ufichuaji wa siri za udukuzi wa mawasiliano ya simu na mtandao unaofanywa na serikali ya Marekani. Kansela Merkel, ambae anakabiliwa na uchaguzi mkuu mwezi Septemba, ameapa kutafuta majibu kutoka kwa Obama kuhusiana na udukuzi huo.
Habari za udukuzi wa mawasiliano ziliwakasirisha raia wengi wa Ujerumani, ambao bado wana kumbukumbu ya kuchunguzwa na serikali chini ya tawala za madikteta wa kinazi na wakomunisti. Wanaharati wameomba ruhusa kwa polisi kufanya maandamano leo, ya kuanzia watu 50 hadi 500, kupinga vitendo hivyo vya idara ya usalama wa taifa ya Marekani NSA.
Merkel alisema katika mahojiano siku ya Jumatatu, kwamba vidokezo vya Marekani viliisaidia Ujerumani kuzuiwa njama za ugaidi, likiwemo jaribio la kuripua maslahi ya Marekani nchini Ujerumani mwaka 2007. Lakini alisema atamuuliza Obama ni kwa kiasi gani mawasiliano ya mtandaoni ya Ujerumani yamekuwa yakidokolewa.
Kiongozi huyo mwenye ushawishi mkubwa zaidi barani Ulaya katika wakati ambapo bara hili linakabiliana na mgogoro wa madeni, pia yuko makini kujadili matarajio ya mapatano ya ushirikiano wa kibishara na uwekezaji kati ya mataifa ya Ulaya na Marekani, TTIP.Vita vya Syria na Afghanistani navyo vinatarajiwa kuchukuwa nafasi kubwa katika mazungumzo yao. Obama na Merkel watazungumza katika mkutano na waandishi wa habari majira ya saa sita mchana.
Tukio kuu la ziara ya Obama
Lakini tukio kuu la ziara yake litakuwa hotuba katika lango lakihistoria la Brandeburg, ambalo wakati mmoja lilikuwa sambamba na ubamba wa ukuta wa Berlin, uliyotenganisha pande mbili za Ujerumani mashariki na magharibi za mji huo mkuu. Mwaka 1987, rais Ronald Reagan alimtaka kiongozi wa Kisovieti kuvunja ukuta huo katika hotuba aliyoitoa akiwa upande wa magharibi wa lango lango hilo.
Merkel alimkataza Obama, wakati huo akiwa Seneta wa jimbo la Illinois, kuzungumza mbele ya lango hilo mwaka 2008. Na badala yake alihutubia wafuasi wake karibu 200,000 katika bustani ya karibu ya Tiergarten. Mwaka huu atasimama katika uwanja wa Pariser, katika upande wa mashariki wa lango hilo, na kutoa wito kwa Ujerumani, Ulaya, na Marekani, kutumia historia yao inayofanana ya ushirikiano imara, kutatua changamoto za karne ya 21.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/dpae,afpe, DW
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman