BERLIN: Watekaji nyara watakiwa kumuachia raia wa Ujerumani
23 Julai 2007Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumanii Frank Walter- Steinmier amewataka kwa mara nyingine tena watekaji nyara nchini Afghanistan kumuachia mateka raia wa Ujerumani wanaemzuilia.
Serikali za Ujerumani na Afghanistan zinashirikiana kitika jitihada za kuachiliwa raia huyo wa Ujerumani.
Wakati huo huo mwili wa mateka mwingine wa Kijerumani uko njiani kuletwa humu nchini.
Maiti hiyo itakapowasili itafanyiwa uchunguzi kubaini chanzo cha kifo chake.
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amesisitiza kwamba serikali yake inaunga mkono jukumu la kikosi cha NATO nchini Afghanistan.
Bibi Merkel amepinga madai ya kundi la Taliban juu ya Ujerumani kuondoa majeshi yake kutoka Afghanistan.
Hatima ya mateka wengine 23 raia wa Korea Kusini ambao pia wanazuiliwa na wapiganaji wa kundi la Taliban bado haijajulikana. Msemaji wa kundi la Taliban amesema kwamba mateka hao wako katika hali nzuri ya afya lakini ameonya kuwa iwapo nguvu zitatumika kutaka kuwaokoa mateka hao basi huenda wakakabiliwa na mashaka.