1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Berlin. Wanajeshi waliojeruhiwa warejeshwa nyumbani.

21 Mei 2007
https://p.dw.com/p/CBzy

Wanajeshi wanne wa Ujerumani waliojeruhiwa katika shambulio la kujitoa muhanga katika mji wa kaskazini mwa Afghanistan wa Kunduz siku ya Jumamosi, wamerejea nyumbani kwa ajili ya matibabu.

Wawili kati yao wako katika hali mbaya. Mwanajeshi wa tano ambaye amejeruhiwa vibaya katika shambulio hilo amebaki nchini Afghanistan.

Shambulio hilo la kujitoa muhanga katika eneo la soko limesababisha vifo vya wanajeshi wengine watatu, na kufikisha idadi ya Wajerumani waliowawa kufikia 21 nchini Afghanistan tangu mwaka 2002.

Wakati huo huo , kiasi cha zaidi ya watu 14 wameuwawa na wengine 30 wamejeruhiwa katika shambulio jingine la kujitoa muhanga katika jimbo la Paktia kusini mwa Kabul.

Wapiganaji wa Taliban wamedai kuhusika na shambulio hilo, ambalo lilitokea wakati magari ya doria ya jeshi la muungano la kimataifa yalipokuwa yakipita katika mji huo wa Gardez.

Baadhi ya ripoti zinasema kuwa wanajeshi wa jeshi hilo la kimataifa ni miongoni mwa waliojeruhiwa.

Kwingineko nchini humo, majeshi ya NATO na yale ya Afghanistan yanasema kuwa yamewauwa wapiganaji 30 wanaosadikiwa kuwa ni wa kundi la Taliban katika shambulio la anga kusini mwa jimbo la Ghazni.