BERLIN : Wadai uchunguzi mpya wa mauaji ya Buback
23 Aprili 2007Maafisa wa serikali ya Ujerumani wametowa wito wa kuanza tena uchunguzi juu ya mauaji ya mwendesha mashtaka wa serikali yaliotokea miaka 30 iliopita.
Wito huo unakuja kufuatia madai ya mwanachama wa zamani wa Kundi la Jeshi Jekundu (Red Army) la wapiganaji wa chini chini kwamba mtu mmoja anaetumikia kifungo kwa uhalifu huo alikuwa hakuhusika na mauaji hayo.Jarida la kila la wiki la Spiegel linaripoti katika toleo lake la leo kwamba lina ushahidi kwamba mwanachama huyo wa zamani wa Red Army Stefan Wisnieswski amempiga risasi na kumuuwa mwendesha mashtaka mkuu wa serikali Siegried Buback.
Lawama ya mauaji hayo kwa muda mrefu imekuwa akitupiwa kwa sehemu fulani mwanchama mwenzake wa msimamo mkali wa kundi hilo Christian Klar ambaye hivi karibuni ameomba msamaha kwa Rais Horst Köhler wa kutaka kuachiliwa baada ya kutumikia kifungo cha zaidi ya miaka 24 gerezani.
Klar alikamatwa hapo mwaka 1982 na kufungwa kwa kuhusika na mauaji kadhaa.
Mashambulizi ya kikatili ya kundi la Red Army kati ya mwaka 1977 na mwaka 1982 yalikuwa yamewalenga watu mashuhuri nchini Ujerumani na kambi za jeshi la Marekani.
Kundi hilo lilivunjwa rasmi hapo mwaka 1998.