1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BERLIN: Wabunge watoa heshima kwa wanajeshi wa kijerumani waliouawa

24 Mei 2007
https://p.dw.com/p/CByj

Wabunge wa Ujerumani walikaa kimya kwa muda mfupi kuwakumbuka wanajeshi watatu wa kijerumani waliouawa jumamosi iliyopita kwenye shambulio la bomu la kujitoa mhanga nchini Afghanistan.

Wanajeshi hao waliuawa pamoja na raia watano wa Afghanistan katika shambulio la bomu la kujitoa mhanga kwenye soko iliyokuwa imejaa watu katika mji wa Kunduz.

Hapo awali misa ya ukumbusho iliandaliwa kwa heshima ya wanajeshi hao baada ya maiti zao kutua kwenye uwanja wa ndege wa kijeshi, mjini Cologne.

Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Franz Josef Jung alisema wanajeshi hao walikuwa wakisaidia ujenzi wa Afghanistan mpya.

Waziri Franz Josef Jung amesema:

"Wanajeshi wetu wanaheshimiwa na umma wa Afghanistan. Wanastahili kuungwa mkono na kushukuriwa kwa kazi wanazozifanya. Kumekuwa na kuaminiana kwa jinsi wanajeshi wetu wanavyotekeleza majukumu yao na kujaribu kuingiliana na wenyeji. Hata hivyo tunatambua, na hili linasikitisha, kwamba kazi yao ni hatari kwa maisha yao"

Waziri Franz Josef Jung amesema Ujerumani itawasaidia maafisa wa Afghanistan kuwakamata na kuwashtaki waliohusika.