1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BERLIN: Uwekezaji ndio utasaidia kupambana na umasikini

9 Mei 2007
https://p.dw.com/p/CC3w

Mawaziri wakuu wa Niger na Togo wamesema,msaada wa kuondolewa mzigo wa madeni umeshindwa kutenzua tatizo la umasikini.Viongozi hao wametoa mwito kwa mataifa tajiri yalioendelea kiviwanda,kuweka vitega uchumi barani Afrika ili nchi masikini zinufaike na utajiri wake wa malighafi.Waziri Mkuu wa Niger Hama Amadou,akizungumza mjini Berlin pembezoni mwa mkutano wa kutayarisha mkutano wa kilele wa nchi tajiri G-8 amesema, msamaha wa madeni nchini mwake haukusaidia kuondosha umasikini.Uwekezaji ndio utaweza kutoa nafasi za ajira na kusaidia nchi zilizo masikini aliongezea Amadou.Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema,suala la misaada kwa bara la Afrika litapewa kipaumbele kwenye mkutano wa kilele wa G-8 utakaofanywa mwezi Juni mjini Heiligendamm.Mnamo mwaka 2005 katika mkutano wa kilele wa G-8 uliofanywa Scotland,nchi 18 zilizo masikini kabisa duniani,zilisamehewa na madola tajiri,madeni ya Euro bilioni 30.