BERLIN: Urusi yataka uhusiano wa kawaida na Uingereza
21 Julai 2007Waziri wa masuala ya nje wa Urusi,Sergei Lavrov amesema,nchi yake inatumaini kusawazisha uhusiano wake na Uingereza.Ametamka hayo wakati wa ziara yake mjini Berlin.Shirika la habari la Urusi, Interfax limemnukulu Lavrov akisema kuwa uhusiano kati ya London na Moscow uwe na msingi wa kuheshimu maslahi ya kila upande.Matamshi hayo yanahusika na hatua ya kufukuza wanadiplomasia 4 wa Kingereza kutoka Moscow sawa na vile Uingereza ilivyofanya kuwafukuza wanadiplomasia 4 wa Kirusi kutoka London.Siku ya Alkhamisi Urusi ilisema, inawafukuza wanadiplomasia wanne wa Uingereza, kufuatia hatua kama hiyo iliyochukuliwa na Uingereza mapema juma hili.Uingereza ilichukua hatua hiyo,baada ya Moscow kukataa kumpeleka Uingereza Andrei Lugovoi,ambae ni mshukiwa mkuu kuhusika na mauaji ya Alexander Litvinenko ambae hapo zamani alikuwa wakala wa Urusi.Litvinenko alifariki kutokana na sumu,Novemba mwaka jana mjini London.