1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BERLIN: Ujerumani yakaribisha pendekezo la Marekani

1 Juni 2007
https://p.dw.com/p/CBw5

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amekaribisha mkakati mpya wa Rais George W.Bush wa Marekani unaohusika na hali ya hewa duniani.Amesema, pendekezo la Bush kwa madola makuu 15,kukubaliana kuhusu suala la gesi zinazochafua mazingira duniani,ni hatua nzuri.Hapo awali,Bush alieleza mkakati wake katika hotuba aliyotoa kabla ya mkutano wa kilele wa madola manane yaliyostawi kiviwanda G-8 utakaofanywa Heiligendamm,nchini Ujerumani juma lijalo.Katika ajenda ya mkutano huo wa kilele,suala lililopewa kipaumbele na Kansela Merkel ni ongezeko la joto duniani. Marekani haikutia saini Mkataba wa Kyoto ambao muda wake humalizika mwaka 2012.Mkataba huo umeweka masharti ya kupunguza uzalishaji wa gesi ya kaboni dayoksaidi ambayo huongeza ujoto duniani.