BERLIN: Ujerumani kuimarisha msaada wa uchukuzi Darfur
15 Septemba 2007Matangazo
Ujumbe wa vikosi vya kimataifa vinavyotazamiwa kupelekwa Darfur,nchini Sudan utaigharimu Ujerumani kiasi cha Euro milioni 130 kila mwaka. Naibu-Waziri wa Nje wa Ujerumani,Gernot Erler amesema,mbali na msaada huo,Ujerumani inataraji pia kuongeza idadi ya wanajeshi wake katika Darfur,ambao hutoa msaada wa uchukuzi kwa njia ya ndege.Wanajeshi hao wanatazamiwa kufikia hadi 200.Hivi sasa,wanajeshi wa Ujerumani wanatoa msaada wa uchukuzi tu.Ujumbe wa amani wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika,utakuwa na wanajeshi 26,000 katika jimbo la mgogoro la Darfur.