BERLIN: Ujerumani inangojea ombi rasmi la Lebanon
6 Septemba 2006Matangazo
Serikali ya Ujerumani ingali ikingojea ombi rasmi kutoka Lebanon kuhusika na mpango wa kupeleka jeshi la wanamaji wake kwenye mwambao wa Lebanon.Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani,Frank-Walter Steinmeier amesema ombi hilo litakapopokewa,ndio uamuzi utapitishwa kwa haraka.Lebanon imesema,kabla ya kufikisha ombi la msaada wa Ujerumani katika Umoja wa Mataifa, inaitaka Israel iondoshe vikwazo vyake vya angani na baharini.Serikali ya Beirut pia inataka manowari za Ujerumani ziwe umbali wa kama maili saba kutoka pwani yake.Sharti hilo limepingwa na mwenyekiti wa majeshi ya Ujerumani,Bernhard Gertz.Amesema,katika hali kama hiyo usafirishaji wa silaha za magendo kwa Hezbollah hautoweza kuzuiliwa sawa sawa.