1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Berlin. Ujerumani imeyataka mataifa ya Ulaya kuwa na msimamo wa pamoja.

22 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCGg

Ujerumani ambayo hivi sasa inashikilia urais wa umoja wa Ulaya , imerudia wito wake wa kuwa na msimamo wa pamoja wa mataifa yote ya Ulaya na NATO kuhusu nia ya Marekani ya uwekaji wa mfumo wa ngao ya ulinzi dhidi ya makombora katika eneo la Ulaya ya kati, wakati Russia imerudia upinzani wake kwa mpango huo.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ameonya kutokea mgawanyiko katika umoja wa Ulaya kuhusiana na suala hilo na kusema kuwa ukosefu wa umoja utadhoofisha umoja huo na kukosa mwelekeo katika uwezo wake wa kusisitiza msimamo wake.

Mpango wa Marekani wa uwekaji wa ngao ya ulinzi dhidi ya makombora nchini Poland na Jamhuri ya Chek, imeleta matamshi makali ya mashambulizi kutoka kwa balozi Russia nchini Ujerumani.

Vladimir Kotenev ameonya kurejea tena kwa mashindano ya silaha.

Russia inapinga kuwekwa kwa mfumo huo ambao Marekani imesisitiza kuwa una nia ya kujilinda dhidi ya vitisho kutoka mataifa kama Iran na Korea ya kaskazini na hauhatarisha hali ya Russia.