1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BERLIN: Schröder na Merkel wapiga kura zao

18 Septemba 2005
https://p.dw.com/p/CEZl

Kansela wa Ujerumani Gerhard Schröder na mpinzani wake wa karibu, Angela Merkel, wamepiga kura zao huku wajerumani wakijitokeza kushiriki katika uchaguzi unaoelezewa kuwa mashindano makali zaidi tangu kumalizika kwa vita vya pili vya dunia.

Akiwa mjini Hannover anakotokea, Schöder akiwa ameandamana na mkewe Doris walipiga kura kwenye kituo kilicho katika shule karibu na nyumbani kwao. Doris ameelezea matumaini yake ya chama cha Social Democrats kushinda uchaguzi, lakini Schöder hakuzungumza na waandishi habari baada ya kupiga kura.

Angela Merkel kwa upandde wake alipiga kura mjini Berlin akiwa ameandamana na mumewe Joachim Sauer, mtaalamu wa kemia.

Kama utamaduni wao waturuki wanaoishi hapa Ujerumani wanampendelea Schröder ambaye amekuwa akitetea Uturuki irihusiwe kujiunga na umoja wa Ulaya. Wanakitazama chama cha SPD kama chama kinachowakaribisha wahamiaji kikilinganishwa na muungano wa CDU-CSU unaongozwa na Merkel. Merkel sio kipenzi cha waturuki kwa kuwa anapinga Uturuki kuwa mwanachama wa umoja wa Ulaya.

Kati ya waturuki milioni 2.6 wanaoishi Ujerumani, nusu milioni wamejiandikisha kupiga kura na uamuzi wao utakuwa muhimu katika kuamua ni nani atakayeibuka mshindi kati ya Schröder na Merkel. Ikiwa wagombea wa ukansela watakaribiana sana katika matokeo, uamuzi wa mwisho utategemea uchaguzi utakaofanyika mjini Dresden tarehe 2 mwezi ujao.