1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BERLIN : Schroeder kutokuwemo katika serikali mpya

12 Oktoba 2005
https://p.dw.com/p/CESs

Kansela Gerhard Schroeder anayeondoka madarakani hapo jana amethibitisha kwamba yumkini hatakuwemo katika serikali mpya ya mseto itakayoongozwa na mpinzani wake kiongozi wa kihafidhina Angela Merkel.

Akizungumzia mazungumzo yanayokuja ya kuunda serikali hiyo kati ya chama chake cha Social Demokrat SPD na kile cha Merkel cha Christian Demokrat CDU Schroeder anataka kushiriki mazungumzo hayo ili kusaidia serikali hiyo ifanikiwe. Amesema hivyo ndivyo alivyoelewa shughuli inayowakabili hata kama hawatakuwemo tena kwenye serikali mpya.

Duru za SPD zilisema hapo Jumatatu kwamba Schroeder aliwaambia hana mipango ya kuwemo kwenye serikali hiyo mpya hata hivyo kumekuwepo na tetesi kwamba SPD kitashinikiza sana kwa Schroeder kuwa makamo kansela chini ya Merkel.

Merkel anatazamiwa kuwa kansela wa kwanza wa kike katika historia ya Ujerumani akiongoza serikali ya kushirikiana madaraka kufuatia makubaliano ya vyama viwili vikuu vya kisiasa nchini.