1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BERLIN. Schroeder kulivunja bunge na kuitisha uchaguzi wa mapema, Lafontaine akihama chama cha SPD.

25 Mei 2005
https://p.dw.com/p/CFAN

Kansela Gerhard Schroeder wa Ujerumani ameungwa mkono na chama chake cha SPD kulivunja bunge na kuitisha uchaguzi mkuu mapema kabla tarehe iliyopangwa hapo awali.

Hapo kabla Schroeder alisema anapanga kufanya kampeni za kibinafsi pasipo kushirikiana na chama cha Greens, ambacho kimekuwa sehemu ya muungano ambao umekuwa ukiitawala nchi hii. Schroeder amesema atawasilisha mswada wa kutokuwa na imani na serikali tarehe mosi mwezi Julai na anataka uchaguzi ufanyike tarehe 18 mwezi Septemba, mwaka mmoja kabla tarehe ya awali.

Chama chake cha Social Democrats kilishindwa vibaya katika uchaguzi wa mkoa wa North Rhine Westphalia Jumapili iliyopita. Chama cha Christian Democrats, CDU, kimeashiria kwamba kiongozi wake Angela Merkel atakuwa mgombea wake wa wadhifa wa kansela katika kinyang´anyiro hicho cha uchaguzi.

Wakati huo huo, kiongozi wa zamani wa chama cha SPD, Oscar Lafontaine, aliyejiuzulu kama waziri wa fedha mwaka wa 1999, ametangaza atakihama cha cha SPD na kuuwakilisha muungano wa upinzani katika uchaguzi ujao. Lafontaine ambaye amekuwa mwanachama wa chama hicho kwa miaka 39, amesema hatua yake hiyo inafuatia mabadiliko ya sheria za wafanyakazi hapa nchini.

Wadadisi wanasema chama kitakachoongozwa na Lafontaine, kitamdhoofisha zaidi kansela Schroeder katika wingi wa kura. Kura ya maoni inaonyesha chama cha SPD kimeshindwa na upinzani.