BERLIN : Schroeder bado ana matumaini ya kushinda uchaguzi
28 Agosti 2005Licha ya kuwa nyuma kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni zikiwa zimebakia wiki tatu tu kabla ya uchaguzi mkuu Kansela Gerhard Schroeder wa Ujerumani amesema leo hii bado ana matumaini kwamba atashinda kwa kipindi kengine madarakani na chama chake cha Social Demokarat SPD na kwamba hana mpango B ( yaani mbadala wa mageuzi).
Ameiambia televisheni ya ZDF kwamba anaendelea na mpango wake A wa mageuzi na kwamba hiyo ina maana kuwania kukifanya chama cha SPD kuwa chenye nguvu kabisa.Uchunguzi wa maoni uliofanywa na Infratest kwa ajili ya televisheni ya ARD nchini Ujerumani umebaini chama cha Schroeder kimejiimarisha kidogo katika siku za hivi karibuni kwa kuungwa mkono kwa asilimia 31 lakini chama cha Christian Demokrat CDU cha Angela Merkel na wenzao Christian Social Union wa jimbo la Bavaria bado vinaendelea kuogoza vizuri kwa kuungwa mkono kwa asilimia 42.
Kumekuwepo na tetesi kubwa kwamba iwapo Bi. Merkel na mwenza waliyemchaguwa kuunda nao serikali ya mseto chama cha Free Demokrat watashindwa kuunda serikali kutokana na kukosa wingi wa viti bungeni CDU huenda badala yake ikaungana na SPD cha Schroeder na kuunda kile kinachojulikana kama muungano mkuu.
Hatua hiyo itamweka Merkel kwenye wadhifa wa Ukansela na kumbwaga nje Schroeder uwezekano ambao Shroeder anaupinga kwa kusisitiza kwamba mpango wake ni kuendelea kutawala kwa kushirikiana na chama cha Kijani.