BERLIN : Schroeder ashindwa kura ya kutokuwa na imani
2 Julai 2005Kansela Gerhard Schroeder wa Ujerumani ameshindwa kura ya kutokuwa na imani na serikali yake aliyoiandaa hapo jana na kuzusha matumaini ya kufanyika uchaguzi na mapema ambao yumkini ukatowa kiongozi wa kwanza wa kike nchini Ujerumani.
Kutokana na matokeo hayo Schroeder amemtaka Rais Horst Köhler wa Ujerumani kuitisha uchaguzi na mapema ikiwezekana mwezi wa Septemba.Schroeder amehalalisha jaribio lake hilo la kutaka uchaguzi na mapema mwaka mmoja kuliko ilivyokuwa imepangwa kwa kusema kwamba kushindwa kwa chama chake chake cha SPD katika uchaguzi wa jimbo la North Rhine Westphalia hapo mwezi uliopita kumeonyesha kwamba haungwi mkono kutokana na sera yake ya mageuzi.
Kiongozi wa upinzani wa kihafidhina Angela Merkel amesema uchaguzi wa mapema ni jambo lisiloweza kuepukwa na kuziita sera za mageuzi za serikali kuwa zisizoeleweka.Ushindi wa wahafidhina hao katika uchaguzi wa Septemba utamfanya Merkel kuwa Kansela wa kwanza wa kike nchini Ujerumani.
Kwa mujibu wa katiba ya Ujerumani Rais Köhler lazima aamuwe hivi sasa iwapo uchaguzi huo wa mapema unaweza kufanyika au la.