BERLIN Schöder atangaza msimamo wake juu ya bajeti ya umoja wa Ulaya
16 Juni 2005Kansela wa Ujerumani Gerhard Schöder ametangaza msimamo wake juu ya bajeti ya umoja wa Ulaya. Katika hotuba yake aliyoitoa mbele ya baraza la chini la bunge la Ujerumani, Bundestag, Schröder ameitolea wito Uingereza kukubali kukiwachilia kiwango cha fedha inachokipokea kutoka kwa umoja huo.
Amesema miaka 20 imepita tangu Uingereza iliporuhusiwa kupokea fedha hizo na uamuzi huo umepitwa na wakati. Amezitolea wito nchi wanachama wa umoja wa Ulaya kuendelea mbele na shughuli za kuiidhinisha katiba ya umoja huo, licha ya kukataliwa na wafaransa na wadachi, na Uingereza kuahirisha kura ya maoni juu ya katiba hiyo.
Habari zaidi zinasema kamati ya bunge inayochunguza kashfa ya utoaji visa, inayomkabili waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Joschka Fischer, imerudia vikao vyake hii leo, licha ya juhudi za serikali kuumaliza uchunguzi huo. Mahakama ya katiba mjini Karlsruhe imesema uamuzi wa serikali kusimamisha kusikilizwa kwa kesi hiyo ilikuwa kinyume cha sheria.