BERLIN: Polisi watoa mchoro wa picha ya mshukiwa wa mauaji
17 Agosti 2007Polisi wametoa mchoro wa picha ya dereva wa motokaa iliyoonekana ikiondoka kwa kasi kutoka eneo la mauaji ya wanaume sita raia wa Italy juzi Jumatano mjini Duisburg, magharibi mwa Ujerumani.
Polisi walipata maiti za wanaume hao zikiwa na majeraha ya risasi vichwani nje ya mkahawa wa kitaliani karibu na kituo cha treni cha mjini Duisburg, Jumatano alfajiri.
Wakati huo huo, polisi nchini Italy wameimarisha usalama katika eneo la kusini la Calabria kufuatia kuuwawa kwa wanaume hao sita katika tukio linalochukuliwa kuwa la uhasama wa kimbari.
Polisi wameyasaka makazi ya kundi la kigaidi la Ndrangheta huku kukiwa na hofu ya visa vya kulipiza kisasi kufuatia mauaji ya wanaume hao.
Wachunguzi wanne wa Italy wamo Ujerumani kusaidia kuchunguza mauaji hayo. Wanaume sita wa Italy kati ya umri wa miaka 16 hadi 39, waliuwawa juzi Jumatano katika mji wa Duisburg.
Waziri mkuu wa Italy Romadno Prodi, amezitetea juhudi za serikali yake katika kupambana na uhalifu, akisema wahalifu 1,000 wamekamatwa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.