1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Berlin. Nafasi ya mwisho ya chama cha SPD kubaki madarakani katika jimbo muhimu hapa Ujerumani, uchaguzi kufanyika Jumapili.

21 Mei 2005
https://p.dw.com/p/CFBm

Kansela wa Ujerumani Gerhard Schroeder amefanya juhudi zake za mwisho kukisaidia chama chake cha Social Democratic kubaki madarakani katika jimbo muhimu la North Rhine-Westphalia.

Wapiga kura katika jimbo hilo wanakwenda kupiga kura kesho Jumapili .

Kushindwa kutamaanisha kuwa muungano unaounda serikali ukiongozwa na Bwana Schroeder utakuwa umedhoofika mno , miezi 16 kabla ya uchaguzi mkuu mwingine nchini Ujerumani.

Chama tawala cha SPD kimelitawala jimbo hilo muhimu kiviwanda na lenye watu wengi nchini Ujerumani kwa muda wa miaka 39. Lakini wapiga kura milioni 13 wanaonekana kutaka kukichagua chama cha upinzani cha Christian Democtaric Union, wakikamilisha mlolongo wa ushindi dhidi ya chama cha SPD katika uchaguzi wa majimbo.

Katika mwaka 1999, chama cha SPD kilitawala katika majimbo 11 kati ya majimbo 16 nchini Ujerumani, lakini kama kitashindwa katika uchaguzi wa Jumapili, kitakuwa kimebakiwa na majimbo matano tu.