BERLIN: Mshukiwa wa ugaidi afikishwa mahakamani
26 Julai 2007Mwanamume mmoja anayeshukiwa kusaidia kuchangisha fedha kwa ajili ya kundi la la-Qaeda nchini Irak na kupeleka wapiganaji wa kigeni nchini humo, amefikishwa mahakamani hapa Ujerumani.
Mwanamume huyo aliye na uraia wa Ujerumani na Moroko, na mkaazi wa mji wa Kiel kaskazini mwa Ujerumani, alikamatwa mnamo mwezi Julai mwaka wa 2006.
Alishtakiwa kwa kuyasaidia makundi ya kigaidi ya kigeni kwa kutuma fedha nchini Misiri na Syria na kuvunja sheria za uuzaji bidhaa nje ya Ujerumani kwa vitendo vyake vya kulisaidia kundi la al-Qaeda kati ya mwezi Agosti mwaka wa 2005 na Julai 2006.
Alipokamatwa mwaka jana, waongozaji mashataka walisema alishukiwa kuwa na uhusiano na Said Bahaji, aliyekuwa na uhusiano wa karibu na marubani wa ndege zilizotumiwa kufanya mashambulio ya mwezi Septemba mwaka wa 2001 nchini Marekani.
Said Bahaji aliishi na kusoma mjini Hamburg hapa Ujerumani.