BERLIN: Mitambo kuukuu ya nishati ya nyuklia ifungwe
1 Septemba 2007Waziri wa Mazingira wa Ujerumani,Sigmar Gabriel anasema,mitambo ya nishati ya nyuklia iliyo ya zamani kabisa nchini Ujerumani,inapaswa kufungwa moja kwa moja.Idadi ya mitambo hiyo ya zamani ni saba.Amesema badala yake,mitambo ya nyuklia iliyo ya kisasa,itaweza kuruhusiwa kufanya kazi muda mrefu zaidi kuliko ilivyopangwa hapo awali.Waziri Gabriel alitamka hayo katika mahojiano yake na gazeti la Süddeutsche Zeitung.
Mwaka huu,mwanzoni mwa majira ya joto,vinu viwili vya zamani vya nishati ya nyuklia,vilipata ajali-kimoja kilipaswa kufungwa na kingine kilishika moto. Kampuni ya Vattenfall iliyokuwa ikiendesha mitambo hiyo miwili,sasa imeanzisha utaratibu mpya wa usalama.Ujerumani ina mradi wa muda mrefu wenye azma ya kufunga mitambo yake ya nishati ya nyuklia.Inatazamia kuwa mitambo yote 17 itakuwa imefungwa ifikapo mwaka 2020.