BERLIN : Merkel hataki muafaka lege lege wa hali ya hewa
3 Juni 2007Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ambaye atakuwa mwenyeji wa mkutano wa viongozi wa Kundi la Mataifa Manane G8 wiki ijayo amezungumzia mkakati mpya wa serikali ya Rais George W. Bush wa Marekani kwa kusema kwamba hatokubali muafaka lelge lege juu ya mabadiliko ya hali ya hewa duniani.
Merkel ambaye anaunga mkono kiwango cha Umoja wa Ulaya cha kupunguza utowaji wa gesi zenye kuathiri mazingira ifikapo mwaka 2050 ameliambia jarida la Spiegel nchini Ujerumani kwamba ni Umoja wa Mataifa inayopaswa kuandaa makubaliano mapya kuchukuwa nafasi ya Itifaki ya Kyoto wakati muda wake utakapomalizija hapo mwaka 2012 na kuendelea.
Ameongeza kusema kwamba magunduzi ya wanasayansi ya jopo la Umoja wa Mataifa hayapaswi kuchujwa.
Mawaziri wa mazingira wa Umoja wa Ulaya wanaokutana katika mji wa zamani wa Ujerumani wa kuzalisha makaa ya mawe wa Essen wametowa wito wa kulenga teknolojia zenye ufanisi wa matumizi ya nishati.