BERLIN : Merkel atetea mpango wa kujumuisha wageni
13 Julai 2007Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amepuuza makundi ya Uturuki yaliosusia makutano wa ngazi ya juu wa kuimarisha ujumuishaji wa wahamiaji kwenye jamii ya Ujerumani hapo jana na kuyashutumu kwa kueneza habari za uongo juu ya sheria mpya za uhamiaji.
Akiuzinduwa mpango mpya wa taifa wa kuwajumuisha wageni katika jamii ambao unajumuisha hatua kama vile kutowa mafunzo zaidi ya lugha na kuwasaidia vijana kujifunza na kupata ajira amezitetea sheria mpya za mpango huo ambao umewakasirisha baadhi ya Waturuki.
Merkel amesema kwamba mpango huo ni hatua ya kupigiwa mfano katika historia ya sera ya kujumuisha wageni nchini Ujerumani na kwamba wakati wakiwasilisha mpango huo nchi na jamii zitowe ushirikiano wao kwa makundi yalioko kwenye jamii pamoja na mashirika kadhalika wahamiaji.
Merkel pia amesema Waturuki hawapaswi kuiwekea serikali muda wa mwisho kutekeleza madai yao na kwamba mlango bado ungali uko wazi iwapo makundi hayo yanataka kujiunga na juhudi hizo za kuwajumuisha kwenye jamii ya Wajerumani.
Makundi matatu makuu ya Uturuki nchini yamaeususia mkutano huo wa kujumuisha wageni kwenye jamii kwa kupinga sheria mpya zilizopitishwa na bunge wiki iliopita zinazotaka pamoja na mambo mengine kuthibitisha kwamba wake au waume zao wanajuwa maneno 200 hadi 300 ya Kijerumani kabla kuhamia nchini.