BERLIN : Merkel ataka uratibu bora wa mipango ya afya
27 Septemba 2007Wafadhili wa Mfuko was Dunia kupambana na UKIMWI, kifua kikuu na malaria wanahudhuria mkutano wa siku moja wenye lengo la kukusanya takriban dola bilioni sita ifikapo mwaka 2010.
Katika hotuba yake ya ufunguzi Kansela Angela Merkel wa Ujerumani akiwa mwenyekiti wa sasa wa Kundi la Mataifa Manane Tajiri duniani ametowa wito wa kuwepo kwa uratibu bora zaidi wa mipango ya afya.Amesema Mfuko huo wa Dunia lazima uambatane na harakati zinazoendeshwa na taasisi nyengine kama vile za Shirika la Afya Duniani na Benki ya Dunia.
Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan ambaye pia amehuhuduria mkutano huo na ni kichocheo cha tokea kuanzishwa kwa mfuko huo hapo mwaka 2002 amesema mpango wa malengo ya milinia wa Umoja wa Mataifa wa kupunguza kiwango cha umaskini kwa nusu ifikapo mwaka 2015 uko nyuma ya wakati hususan katika kushughulikia maradhi.
Hadi sasa mfuko huo umetowa msaada kwa wagonjwa milioni moja nukta moja wa UKIMWI na wagonjwa milioni 3.3 wa kifua kikuu pamoja na mamilioni ya vyandaruwa vya kujikinga na mbu.