1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BERLIN: Merkel akataa masharti ya watekaji nyara

20 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCHB

Kansela wa Ujerumani, Bi Angel Merkel, amekataa kutimiza masharti ya magaidi wa Irak wanaowazuilia Wajerumani wawili.

Watekaji nyara hao wametishia kumuua mama wa kijerumani mwenye umri wa miaka 61 pamoja na mwanawe wa kiume ikiwa wanajeshi wa Ujerumani wataendelea kubakia nchini Afghanistan.

Katika ziara fupi nchini Italia, kansela Angela Merkel amesema Ujerumani haitatishwa na watekaji nyara hao. Hata hivyo kiongozi huyo amesema serikali yake mjini Berlin inafanya kila iwezalo kuwaokoa wajerumani hao.

Jana kansela Merkel alikutana na rais wa Afghanistan, Hamid Karzai, mjini Berlin. Rais Karzai aliishukuru Ujerumani kwa kupeleka ndege sita aina ya tornado kusaidia juhudi za kudumisha usalama nchini Afghanistan.

´Bi kansela nakushukuru kwa kututumia ndege za tornado kupiga picha Afghanistan. Umuhimu wa wanajeshi na ndege hizi sio katika mapigano bali zinawahakikishia Wafghanistan ulinzi na usalama kisaikolojia.´

Rais Hamid Karzai alimwambia Bi Merkel kwamba kutimiza masharti ya watekaji nyara kutaongeza matumizi ya nguvu na ugaidi nchini Afghanistan.

Muda uliowekwa na watekaji nyara hao kabla kumuua Hannelore Krause na mwanawe wa kiume unakaribia kumalizika.