BERLIN: Mdahalo kati ya Schroeder na Merkel
5 Septemba 2005Kansela Gerhard Schroeder na mshindani wake katika uchaguzi mkuu wa Ujerumani,Bibi Angela Merkel wamekabiliana katika mdahalo uliotangazwa kwenye televisheni na uliotazamiwa kuwavutia hadi watazamaji milioni 20.Wagombea uchaguzi hao 2 walipambana kuhusu masuala kadhaa,suala kuu likiwa ni njia ya kuongeza nafasi za kazi na kuchangamsha uchumi wa Ujerumani uliozorota.Kwa maoni ya wadadisi,mchuano huo ni kampeni itakayoweza labda kuwasaidia wapiga kura wanaosita-sita,kujiamulia vipi watapiga kura zao,zikibakia wiki mbili tu kabla ya kufanywa uchaguzi.Uchunguzi wa maoni uliofanywa baada ya kumalizika mdahalo huo,umeonyesha kuwa watazamaji wengi wamehisi kwamba Kansela Schroeder alishinda mchuano huo.Wachambuzi wanasema ingawa matokeo ya mdahalo huo hayawezi kushawishi sana matokeo ya uchaguzi wa Septemba 18,lakini mdahalo huo huenda ukaamua kama muungano ambao Bibi Merkel anatazamia kuunda pamoja na chama cha Free Democrats utaweza kushinda kura za kutosha na kuwa na uwingi wa kutawala.