BERLIN : Mateka wa Ujerumani yungali hai
22 Julai 2007Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter Steinmeir amesema mmojawapo ya Wajerumani wawili waliotekwa nyara nchini Afghanistna wiki hii inaaminika kuwa yungali hai na mwengine amefariki na kwamba hakuuliwa.
Mapema hapo jana kundi la wanamgambo wa Taliban lilidai kuwa limewauwa Wajerumani hao wawili pamoja na Waafghanistan watano waliokuwa wakiwashikilia mateka.
Steinmeir alizungumza na waandishi wa habari mjini Berlin baada ya mkutano wa kamati ya masuala ya dharura ya serikali amesema wanaweza kusema kwamba mmojawapo wa mateka amekufa lakini hakuna kinachodokeza kwamba aliuwawa kila kitu kinashiria kwamba alikufa kutokana na mazingira aliyokuwa akishikiliwa na watekaji wake.Amesema kinachopaswa kufanywa sasa ni kuchukuwa kila hatua inayowezekana kibinaadamu kuokowa maisha ya mateka wa pili.
Wajerumani hao wawili na wenzao watano wa Afghanistan walitekwa nyara katikati ya Afghanistan ambapo walikuwa wakifanya kazi katika mradi mmoja wa bwawa.
Kundi la Taliban mapema lilitishia kuwauwa Wajerumani hao venginevyo serikali ya Ujerumani inaondowa wanajeshi wake 3,000 kutoka Afghanistan ambapo wanatumika chini ya kikosi cha Umoja wa Kujihami wa Mataifa ya Magharibi NATO.
Taliban pia wanatishia kuwauwa mateka 23 kutoka Korea Kusini waliotekwa tafauti hapo Alhamisi.