BERLIN : Mataifa ya magharibi yamuunga mkono Rais Abbas
15 Juni 2007Ujerumani ambayo hivi sasa inashikilia urais wa kupokezana wa Umoja wa Ulaya imelaani kutwaliwa kwa nguvu kwa Ukanda wa Gaza na wanamgambo wa Kipalestina wa kundi la Hamas.
Msemaji wa serikali mjini Berlin amewaambia waandishi wa habari kwamba Rais Mahmoud Abbas wa Palestina anaungwa mkono kikamilifu na Umoja wa Ulaya.Pia ameelezea wasi wasi mkubwa juu ya hali ya kibinaadamu huko Gaza.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Condoleezza Rice pia ameutetea uamuzi huo wa Abbas wa kuvunja serikali ya umoja wa kitaifa ya Palestina na kusisitiza uungaji mkono wa Marekani kwa kiongozi huyo wa Wapalestina.
Rais Abbas wa Palestina tayari amemteuwa Waziri wa Fedha Salam Fayyad ambaye hana ufuasi wa vyama kuwa waziri mkuu mpya.Fayyad ambaye anaheshimika sana na jumuiya ya kimataifa anachukuwa nafasi ya Ismael Haniyeh ambaye ametimuliwa na Abbas hapo jana baada ya kundi la Hamas kuutwaa Ukanda wa Gaza kwa kutumia nguvu.
Fayyad anatazamiwa kuchaguwa mawaziri wapya masaa machache yajayo.
Hata hivyo Waziri Mkuu Haniyeh ameupinga uamuzi wa Abbas na kusema kwamba hatoutekeleza wakati kundi lake la Hamas ikidhibiti Ukanda mzima wa Gaza na kundi la Abbas la Fatah likidhibiti Ukingo wa Magharibi.
Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Kiarabu wanakutana mjini Cairo Misri leo hii kujadili mgogoro huo unaotishia kuwagawa Wapalestina.