BERLIN: Marekani yadai kuwepo silaha kutoka Iran nchini Afghanistan
14 Juni 2007Matangazo
Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Robert Gates, amesema silaha kutoka Iran zinatumika nchini Afghanistan.
Robert Gates, ambaye hapo awali hajaishutumu Iran moja kwa moja, amesema uchunguzi wa hivi karibuni umeonyesha baadhi ya silaha zinazotumiwa na wanamgambo nchini Afghanistan zinatoka Iran.
Hata hivyo waziri huyo amesema hajapata ushahidi kwamba serikali ya Iran inahusika.
Waziri Robert Gates alikuwa akizungumza na waandishi wa habari katika kituo cha kijeshi cha Ramstein nchini Ujerumani akiwa njiani kuelekea Brussels anakotarajiwa kushauriana na mawaziri wenzake wa NATO kuhusu Afghanistan na pia kituo cha kukinga makombora kilichopendekezwa kujengwa katika Ulaya Mashariki.