BERLIN: Maafisa wa Afghanistan wathibitisha kutekwa nyara kwa mjerumani
5 Julai 2007Maafisa wa Afghanistan wamethibitisha kuwa raia wa Ujerumani ametekwa nyara nchini Afghanistan. Gavana wa jimbo la Nimroz kusini magahribi mwa Afghanistan, amesema mjerumani huyo alitekwa nyara katika wilaya ya Delaram katika mkoa wa Farah kwenye mpaka na jimbo la Nimroz.
Hapo awali wizara ya mashauri ya kigeni ya Ujerumani mjini Berlin, ilitangaza kutekwa nyara kwa mjerumani huyo.
Msemaji wa wizara hiyo amesema mwanamume wa kijerumani alipotea tangu Alhamisi wiki iliyopita. Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Franz Josef Jung amesema juhudi zimeanza kumuokoa raia huyo.
´Habari tulizonazo ni kwamba mmoja wetu ametekwa nyara kusini mwa Afghanistan na tunajukumu la kufanya juhudi kwa haraka kumuokoa.´
Imeripotiwa kuwa mjerumani huyo aliyetekwa nyara si mwanajeshi, mwandishi wa habari wala mfanyikazi wa shirika la kutoa misaada.