1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BERLIN : Kikosi cha Ujerumani kwa Lebanon chaidhinishwa

20 Septemba 2006
https://p.dw.com/p/CDAc

Bunge la Ujerumani leo limeidhinisha mpango wa serikali wa kutuma wanajeshi 2,400 nchini Lebanon na kuondowa pingamizi ya mwisho kwa shughuli za kulinda amani ambazo Kansela Angela Merkel amezielelezea kuwa za kihistoria.

Wabunge 442 walipiga kura kuunga mkono mpango huo na152 walipinga wakati watano walijitowa kupiga kura.Vyama viwili vya upinzani kile cha Free Liberal Demokrat FDP na kile cha Left Party walielezea mashaka yao kabla ya kupigwa kwa kura hiyo kwa kusema kwamba kuna hatari kwamba wanajeshi wa Ujerumani wakapambana na wanajeshi wa Israel jambo ambalo linaonekana kuwa ni tatizo kwa kuzingatia hisoria ya Manazi ya Ujerumani.

Kikosi cha wanajeshi 1,000 wa Ujerumani kinatazamiwa kuondoka kwenye mji wa bandari wa kaskazini wa Wilhelmshaven hapo Alhamisi.Wanajeshi wa Ujerumani wataongoza kikosi cha majini kupiga doria kwenye mwambao wa Lebanon kuzuwiya usafirishaji wa shehena za silaha kwa wapiganaji wa Hizbollah.