BERLIN : Jung na utata wa makombora ya Marekani
26 Aprili 2007Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Josef Jung apunguza makali utata juu ya mipango ya Marekani ya kuweka makombora ya kujihami katika Ulaya ya mashariki.
Kufuatia mkutano wake na Waziri wa Ulinzi wa Marekani Robert Gates mjini Berlin Jung amesema anathamini ahadi ya Marekani kuendelea kuijulisha Ujerumani juu ya maendeleo ya mipango yao hiyo hatua kwa hatua.
Hata hivyo Urusi inaendelea kupinga vikali wazo la kuwa na makombora ya ulinzi ya Marekani katika nchi za Poland na Czeck. Gates amesisitiza pendekezo la Marekani la kushirikiana na Urusi data za makombora ya kutowa tahadhari pamoja na teknolojia ya mfumo huo wa makombora ya kujihami.
Serikali ya Marekani inasema makombora hayo ya kujihami yanahitajika kuilinda Marekani dhidi ya uwezekano wa mashambulizi ya makombora kutoka Mashariki ya Kati.