Benki za jamii Tanzania zina wakati mgumu
11 Januari 2018Ingawa hali ya kisiasa ya Tanzania imekuwa nzuri kwa biashara za benki, benki nyingi za kizalendo zilizoundwa katika miaka ya karibuni, hupata shida. Kipengele muhimu zaidi katika matatizo ya nchi hii kimekuwa uchumi wa mashambani usioendelea, ukiwa umegubikwa na umasikini. Katika hali hiyo, ni muhimu kwa watendaji katika sekta ya kilimo kuzalisha ziada ambayo benki hizo zinaweza kuwekeza; vinginevyo mfumo wa benki utakuwa ule wa kuhamisha fedha tu.
Hadi sasa ni kampuni chache za ndani zinafanya biashara nje ya mji au mkoa ambapo zimeanzishwa. Zile zenye ujuzi wa biashara zinapanuka kwenda maeneo mengine zaidi kupata masoko ya bidhaa na huduma zao. Katika mchakato huo, pia zinakusanya rasilimali za uzalishaji bidhaa kutoka maeneo tofauti kwa kushirikiana na benki.
Kama vile maisha ya wanyama yanavyohitaji oksijeni kupumua, benki na shughuli nyingine za kibiashara zinahitaji fedha ili zidumu. Maisha na biashara zenye mafanikio hutegemea mfumo bora wa benki. Nchini Tanzania, hata hivyo, baadhi ya watu hufanya shughuli zao kama vile wamekata tamaa ili mradi wapate wanachotaka.
Mambo wanayofanya ni pamoja na uvuvi haramu, ulaghai wa bidhaa, usafirishaji haramu wa binadamu, uchimbaji wa madini bila leseni, ujangili, na kutengeneza fedha bandia. Mambo hayo hupotosha taswira ya nchi wakati rushwa imekuwa njia ya kawaida kwa baadhi ya viongozi kujaza mifuko yao.
Katika hali hiyo, bila kujali uwazi wa benki katika shughuli zifanyazo, bila shaka zitapata taabu kuendelea kifedha bila kuzama.
Benki Kuu ya Tanzania ilipotangaza juma lililopita kuwa imefuta leseni za benki tano za jamii na kuziweka nyingine tatu chini ya uangalizi kwa miezi sita, ilipeleka mawimbi ya mshtuo kwa benki nyingine lakini swali moja lilibakia. Je, itachukua muda gani kabla ya asasi binafsi nyingine zaidi zinazotoa huduma za kifedha kukumbwa na maradhi hayo hayo yatokanayo na mtaji mdogo?
Tangazo la benki kuu huenda lilizishtua benki hizo ni kuzibwaga katika hali ya kufadhaika kibiashara mwanzo wa mwaka mpya.
Mikopo kwa makundi ni motisha
Lakini wenye amana katika benki na umma kwa ujumla hutarajia benki zipate pesa wakati wote – kutokana na ada kwa shughuli zao, kwa kushauri kampuni mbalimbali na wateja binafsi, viwango vya riba juu ya mikopo, ulinzi wa mali na uwekezaji katika miradi inayotoa faida.
Benki ndogo ndogo za Tanzania hazijapiga hatua ya kujisifia katika kutegemeza biashara ndogo za ndani na hata kuwepo kwa benki hizo ni nadra kujulikana kwa umma. Baada ya kufungua milango kwa wateja, inaelekea kuwa mameneja wa benki hizi walitarajia mtiririko wa pesa kuingia kirahisi kwenye hifadhi za benki.
Hawakujali wateja wao watarajiwa, ikiwa ni pamoja na wazalishaji wadogo wadogo wa viwanda, wakulima wadogo na miradi ya vijana ambao huhitaji mikopo ili iwasaidie kuongeza uzalishaji.
Mikopo kwa makundi hayo ingekuwa motisha ya kuinua mapato na uwekezaji wa moja kwa moja katika mlolongo wa kuongeza thamani za bidhaa na kukuza kipato cha watu wa kawaida.
Biashara ya benki siyo sawa na kusimamia chama cha akiba na mikopo, kama wanavyofikiri waanzishaji wa benki za jamii. Katika uwanja wa soko huria, benki zinaanzishwa zikiwa na malengo maalum ya kukuza kampuni na uwajibikaji imara kwa wanahisa pamoja na umma zinaohudumia kwa jumla.
Kuanguka kwa benki ndogo za jamii, hata hivyo, kusiwe ishara ya habari mbaya kwenye nyumba za fedha zilizobaki kwamba ziko karibu kuporomoka. Ni kweli kwamba hivi karibuni shughuli za kibiashara zimedorora kutokana na udhibiti mkali wa fedha kutoka serikalini, lakini hili ni jambo la muda.
Benki tatu kati hizo zilizofungwa -- Njombe Community Bank Limited, Kagera Farmers Cooperative Bank Limited na Meru Community Bank Limited - ziko katika maeneo mazuri ya kilimo ambako wakulima wanahitaji ushauri wa kitaalam kuhusu mazao ya biashara yanayofaa walime. Wakati huu wengi wao wamekatishwa tamaa na kushuka kwa bei za mazao ya biashara, hasa kahawa.
Wajasiriamali wa Tanzania hawapaswi kuona kufungwa kwa benki hizo kama mwisho wa jitihada binafsi za kuanzisha benki za jamii, ambazo zinalenga kukuza ustawi wa uchumi.
Zikiwepo rasilimali za kutosha na mipango sahihi, benki hizi zinaweza kuweka alama isiyofutika katika ustawi wa watu na kufungua njia mpya za kukuza biashara. Zinahitaji menejimenti ya kitaalam na uongozi usio na tamaa ya kujilimbikizia mali.
Mwandishi: Anaclet Rwegayura
Mhariri: Iddi Ssessanga