1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Benki ya dunia yakosolewa kuhusu haki za binaadamu

Admin.WagnerD22 Julai 2013

Human Rights Watch imesema benki ya dunia imefumbia macho hatari zinazozikabili haki za binaadamu za watu inaolenga kuwasaidia, kutokana na kutokuwa na mifumo imara ya kuzuia ukiukaji wa haki hizo.

https://p.dw.com/p/19Bhs
Human Rights Watch Kenneth Roth.
Human Rights Watch Kenneth Roth.Picha: dapd

Ripoti ya kurasa 59 iliyopewa jina "Maendeleo yasiyotumiwa vibaya- Jinsi benki ya Dunia inavyoweza kuzuia ukiukaji wa haki za binaadamu," inayotokana na utafiti wa Human Rights Watch kutoka sehemu mbalimbali duniani imebainisha madhara yanayowapata baadhi ya watu walio katika hatari zaidi kutokana na miradi inayofadhiliwa na benki ya dunia.

Rais wa benki ya dunia, Jim Yong Kim.
Rais wa benki ya dunia, Jim Yong Kim.Picha: REUTERS

Katika ripoti hiyo, Huma Right Watch iliaangazia kesi tatu, moja kutoka Vietnam na mbili kutoka nchini Ethiopia, kuonyesha ni jinsi gani benki hiyo isivyotambua hatari ya ufadhili wake kwa haki za binaadamu, au kutochukua hatua zozote kutatua matatizo hayo.

"Benki ya dunia hutoa mabilioni ya dola kila mwaka kusaidia juhudi za maendeleo duniani kote. Hiki ni kiasi kikubwa sana cha pesa, lakini kinachostajaabisha ni kwamba benki ya dunia haikakikishi kuwa fedha hizi hazichangii katika ukiukaji wa haki za binaadamu," amesema Jessica Evans, Mtafiti mkuu kutoka Human Rights Watch.

Human Rights Watch imesema malengo iliyojiwekea benki ya dunia hivi karibuni, ya kukomesha umaskini uliokithiri na kuendeleza mafaniko kwa wote yanahusiana kwa karibu na haki ya kila mtu kuishi maisha yanayostahili, kwa kuwa na upatikanaji wa chakula, maji na makaazi mazuri.Lakini linasema shirika hilo lenye makao yake jijini New York Marekani, kuwa malengo hayo hayawezi kutimia bila ya benki hiyo kuhakikisha kuwa inalinda haki za watu inaotaka kuwasaidia.

Ufadhili unaochochea ukiukaji wa haki

Human Rights Watch imesema katika kesi nyingi, benki ya dunia imeshindwa ama kutambua au kutatua hatari za haki za binaadamu katika programu zake, na matokeo yake kwa mfano nchini Vietnam, benki hiyo imefadhili programu katika vituo vya serikali wanakozuiliwa watumiaji wa dawa za kulevya, ambamo Huma Rights Watch imebaini kuwepo vitendo vya watu kufungwa kiholela, kulaazimishwa kazi, kuteswa na aina nyingine za ukiukaji wa haki zao.

Waziri mkuu wa Ethipia, Haile Mariam Desalegne.
Waziri mkuu wa Ethipia, Haile Mariam Desalegne.Picha: CC-BY-SA- World Economic Forum

Nchini Ethiopia, serikali ilipokea mkopo wa dola bilioni mbili kusaidia sekta za elimu, afya na miradi ya maendeleo. Lakini mradi katika mkoa wa magharibi wa Gambella, unaohusisha kuhamisha watu milioni 1.5 wenyeji na watu wengine wanaotengwa, umekumbwa na vurugu zinazowahusisha wanajeshi walio na jukumu la kuwahamisha watu kutoka katika vijiji vyao.

"Walikuja kwa baba yangu wakasema tunakutaka uhamie katika ardhi nyingine. Baba yangu alisema asingehamia huko. Siku iliyofuata, wanajeshi walikuja wakaaza kumpiga kila mtu, na kuwalaazimisha watu kuhamia katika makaazi mapya, na walichoma vibanda vyetu, alisema mkaazi mmoja wa Gambella akitoa ushuhuda wake kwa Human Rights Watch.

Huma Rights Watch imetoa wito kwa benki ya dunia kuboresha viwango vya haki za binaadamu iliyojiwekea, kutimiza majukumu yake ya kisheria kuhakikisha kuwa haki za binaadamu zinaheshimiwa katika miradi yake.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/dpa, HRW
Mhariri; Yusuf Saumu