1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Benki ya Dunia na mikakati ya kudhibiti matumizi mabaya ya fedha

Charles Hilary5 Juni 2006

Nyaraka iliyovuja kutoka Benki ya Dunia,zimeonesha jitahada rasmi zaharakati kwa ajili ya kutafuta njia za kukabiliana na ufisadi pamoja na ulaji rushwa unaofanywa katika miradi ya benki hiyo,bila ya kuwepo vikwazo kwa taasisi za fedha.

https://p.dw.com/p/CHnD
Rais wa Benki ya Dunia Paul Wolfowitz.
Rais wa Benki ya Dunia Paul Wolfowitz.Picha: AP

Nyaraka hiyo inaeleza kuwa Benki ya Dunia yenye makao yake makuu mjini New York,inatakiwa kuweka msimamo unaoeleweka kwa ajili ya kusimamia fedha hizo na kupambana na ulaji rushwa na pia inawajibika kuwa na mfumo wa ndani wa kisheria wa kushauri namna ya kuendelea na mchakato wa kupambana na rushwa iliyotapakaa duniani,kwa ajili ya kuepuka kupoteza hadhi yake.

Kwa mujibu wa nyaraka hiyo iliyopatikana kutoka ofisi ya makamu wa rais wa benki ya dunia,inamnukuu Rais wa benki hiyo Paul Wolfowitz,ambaye ni hivi karibuni alitoa matamshi yenye msimamo mkali ya kupambana na vitendo vilivyokithiri vya rushwa.Pia ndani yake kuna maoni kutoka kwa wakurugenzi wakuu wa benki ya dunia na maofisa wengine waandamizi wa benki hiyo,yanaoelezea hatua za siku za baadae na sera za kupambana na vitendo vya rushwa.

Ndani ya nyaraka hiyo imeelezwa changamoto wanayokabiliana nayo maofisa ndani ya benki ya dunia,tangu Bwana Wolfowitz aliposhika nafasi ya kuiongoza benki hiyo kubwa ulimwenguni na kuanzisha kampeni iliyoungwa mkono kwa kiasi kikubwa na vyombo vya habari duniani wakati ule wa mkutano uliofanyika mwezi wa Aprili uliowakutanisha pamoja na maofisa wa shirika dada la fedha duniani IMF.

Wakati wa ziara yake ya hivi karibuni aliyoifanya nchini Indonesia,Bwana Wolfowitz alitangaza mikakati yake ya muda mrefu ya kutumia fedha za benki hiyo pamoja na wataalam wake,kusaidia nchi zinazoendelea ili serikali zao zibanwe kuachana na michezo michafu inayofanywa na baadhi ya maofisa wake ya kuchukua mirungura pamoja na kujihusisha na vitendo vingine visivyopendeza vya ufujaji wa fedha.

Suala muhimu ndani ya mpango huo ni kuundwa kwa kikosi cha kupambana na rushwa katika nchi nyingi ambapo ofisi za benki ya dunia zipo.

Pia Bwana Wolfowitz ana mipango ya kuweka muundo mpya katika Idara ya uadilifu ya benki hiyo,ambayo itakuwa na jukumu la kuangalia nyendo za matumizi ya fedha za benki hiyo pamoja na uendeshaji mzima unakuwa katika hali ya uadilifu zaidi.

Mwezi wa Februari,Rais huyo wa Benki ya Dunia,aliongoza jitahada za kuwakusanya pamoja wakuu wa taasisi nyingine za fedha kama Benki ya Amerika na Benki ya Maendeleo ya Afrika,ili wajifunge kwa kauli kukubali kuendelea kupambana na vitendo vya rushwa.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa mwaka juzi wa 2004 na kamati ya Seneti ya Marekani,Benki ya Dunia imekwishapoteza kiasi cha dola bilioni 100 zilizokusudiwa kwa maendeleo ya mataifa masikini zaidi duniani,kutokana na kukithiri vitendo vya rushwa tangu mwaka 1946.

Wataalam wengine wamekadiria kuwa kati ya asilimia tano na 25 ya dola bilioni 525,ambazo benki ya dunia imetoa kama mkopo tangu mwaka 1946 zimetumiwa vibaya.Hiki ni kiwango kinachofikia kati ya dola bilioni 26 hadi dola bilioni 130.

Hadi sasa kuna zaidi ya makampuni 330 pamoja na watu binafsi ambao wameshazuiwa kufanya shughuli zozote za kibiashara na Benki ya dunia na majina yao pamoja na shughuli zao zinapatikana katika tovuti ya benki hiyo.