1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Benjamin Netanyahu ziarani mjini Berlin

8 Aprili 2011

Kansela Angela Merkel ahiimiza mazungumzo ya amani kati ya Israel na Palastina yaendelezwe na kushadidia umuhimu wa ufumbuzi wa madola mawili

https://p.dw.com/p/10pni
Kansela Angela Merkel(kulia) na waziri mkuu wa Israel B.NetanyahuPicha: dapd

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amefanya mazungumzo pamoja na kansela wa Ujerumani, Angela Merkel mjini Berlin. Mazungumzo hayo yametuwama katika suala la upepo wa mageuzi katika ulimwengu wa kiarabu na utaratibu wa amani ya Mashariki ya kati.

Hakujakuwa na dalili yoyote ya mvutano wakati wa mazungumzo kati ya kansela Angela Merkel na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu. Hajawahi kuhisi kana kwamba anafadhaika anapokutana na kiongozi mwenzake wa Israel, amesema kansela Angela Merkel na kuzisuta wakati huo huo ripoti zinazodai eti mvutano umezuka miezi ya hivi karibuni kati ya viongozi hawa wawili. Inasemekana eti kansela Angela Merkel alizungumza kwa simu wiki chake zilizopita na Benjamin Netanyahu na kumtuhumnu hafanyi vya kutosha kuendeleza mazungumzo ya amani. Na jana pia kansela Angela Merkel amezungumzia umuhimu wa kupatikana maendeleo katika mazungumzo ya amani na kusema:

"Mkwano lazima umalizike na lengo liwe ufumbuzi wa madola mawili, haki ya kuwepo taifa la kiyahudi la Israel na taifa la Palestina."

Friedensbewegungen in Israel
Wanaharakati wa vugu vugu la Israel la wanaopigania amani kati ya Israel na PalastinaPicha: Peace Now Movement

Lakini vipi hali hiyo ya mkwano itaweza kuepukwa, haijulikani, na Benjamini Netanyahu hakusema chochote. Badala yake amejibu suala la mmojawapo wa waandishi habari wa kiisrael waliofuatana nao akisema :

"Suala hilo nitalizungumzia katika hotuba kadhaa nitakazotoa hivi karibuni. Nakusihini kwa hivyo, muisubiri hotuba yangu."

Kuhusu suala la ujenzi wa makaazi mapya, waziri mkuu wa Israel amesema anaamini suala hilo linaweza kupatiwa ufumbuzi ikiwa amani, usalama na utulivu utapatikana. Ameonya hata hivyo katika wakati ambapo upepo wa mabadiliko unapiga Mashariki ya kati, nchi yake inabidi iwe macho. Anasema wimbi la mageuzi katika ulimwengu wa kiarabu linaweza kuzusha kitisho pia kwa Israel.

Israel Palästina Gaza Grenze
Mpaka unaoitenganisha Israel ,Palastina na GazaPicha: AP

Wakati huo huo, wafuasi wawili wa tawi la kijeshi la Hamas-Ezzedine Qassam, wameuliwa hii leo, wakati jeshi la wanaanga la Israel lilipotupa mabomu karibu na Khan Younes, kusini mwa Gaza. Opereshini hiyo ya kijeshi imeifanya idadi ya waliouwawa kufikia sabaa na 37 kujeruhiwa, tangu madage ya Israel yalipoanza kuishambulia Gaza, kulipiza kisasi kwa shambulio la kombora lililofyetuliwa jana dhidi ya basi moja la wanafunzi kusini mwa Israel. Mwanafunzi mmoja wa kiisrael alijeruhiwa wakati wa shambulio hilo.

Mwandishi:Marx Bettina/Hamidou Oummilkheir

Mhariri:Josephat Charo